Author Archives: admin

SHIRIKA LA MAENDELEO LA USWISI (SDC) LATEMBELEA VIKUNDI VYA WAKULIMA WADOGO

Ugeni kutoka shirikia la maendeleo la Uswisi (SDC) umetembelea vikundi vya wakulima wadogo ambao ni wanachama wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) katika wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro. Lengo la ugeni huu ni kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na MVIWATA. Ugeni huo ulitembelea  vijiji vya Maduhu, Mvumi na Rudewa Gongoni.

Wageni walijionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na wakulima wadogo kupitia MVIWATA. Wanachama walieleza namna MVIWATA ilivyowasaidia kwa kuwapa mafunzo mbalimbali kama vicoba, ujasiriamali, sheria za ardhi, haki za watoto na wanawake na kilimo cha umwagiliaji. Mafunzo ambayo yamewajengea uwezo na yamewasaidia kujikwamua kiuchumi, ambapo wameitaka MVIWATA kuendelea kutoa mafunzo ili yawasaidie zaidi.

Wageni wamefurahishwa na namna ambavyo MVIWATA inafanya kazi zake kwa kutetea maslahi ya wakulima wadogo kwa kuhakikisha kwamba mkulima mdogo ana nufaika.

MVIWATA YAFANYA UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI WA KAMATI ZA UMAPESA, KATA YA KISAKI, MOROGORO VIJIJINI.

Mtandao Wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) umefanya zoezi la ufuatiliaji wa utekelezaji wa kamati za UMMAPESA (PETS) yaliyotolewa kwa wakulima 124 katika Kata ya Kisaki, Wilaya ya Morogoro Vijijini.

Ufuatiliaji huo umefanyika katika vijiji vinne vya Kisaki station, Nyarutanga, Gomero na Kichangani. Ufuatiliaji ulilenga kubaini changamoto za utekelezaji wa UMMAPESA na kutafuta suluhisho za changamoto zilizojitokeza kwa ustawi endelevu wa wananchi.

Katika ufuatiliaji wakulima wameeleza hatua walizofikia na changamoto walizokumbana nazo katika ufuatiliaji wa miradi mbali mbali inayoendelea katika vijiji vyao

Awali kabla ya kuelezea changamoto za ufuatiliaji huo, wakulima walibainisha miradi mbali mbali waliyokuwa wakiifuatilia kama ifuatavyo; miradi ya maji, uvunaji wa mbao, ujenzi wa nyumba za waalimu, ujenzi wa nyumba za madaktari, ujenzi wa nyumba za madaktari, ujenzi wa ofisi za vijiji na ujenzi wa vyoo katika shule za msingi.

Katika kuelezea changamoto hizo, ushirikiano hafifu baina ya viongozi wa serikali za vijiji na uelewa mdogo wa wanakijiji katika kutambua umuhimu wa mkutano mkuu wa kijiji kama msingi mkuu wa maamuzi ya maendeleo ya kijiji kumechangia kwa kiasi kikubwa katika ubadhirifu wa mali za umma.

Ushirikiano mbaya kati ya viongozi wa serikali ya mkoa, wilaya na vijiji katika kubuni na kutekeleza miradi ilikuwa ni changamoto nyingine iliyoibuka katika ufuatiliaji huo. Hatua hiyo imepelekea viongozi wa vijiji pamoja na wanakijiji kutokuwa na taarifa sahihi za miradi mbali mbali inayoendelea katika vijiji vyao hivyo kukosa taarifa za miradi ambayo imesimama kwa mda mrefu katika vijiji vyao na kutokujua ni lini miradi hiyo itakamilika.

Licha ya changamoto zote hizo walizokumbana nazo, wakulima hao wameishukuru taasisi ya MVIWATA katika kutoa elimu ambayo imewafungua macho ya kuhoji, kupata taarifa na kuona jinsi wanavyoweza kunufaika na miardi mbali mbali inayoendelea katika vijiji vyao. Pia wamesisitiza kuendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu miradi hiyo pamoja na kuendelea kusambaza elimu ya uraia kwa wananchi wengine ili kujua haki na wajibu wao kama raia.

Wakihitimisha mawasilisho yao, wakulima hao wameazimia kuendelea kuwaelimisha wananchi wengine katika maeneo yao ili kutambua umuhumu wa kuhudhuria mikutano mikuu ya kijiji kwa sababu nidpo mipango ya maendeleo na taarifa mbali mbali za kimaamuzi zinapopatikana, hivyo ushiriki wao utawapa nafasi ya kuhoji mambo mbali mbali yanayoendelea katika vijiji vyao.

Mwisho wameiomba MVIWATA kuendelea kuwapa elimu ya uraia ambayo imewasaidia kupata njia bora za ufuatiliaji wa mali za umma pamoja na ushiriki wao katika maendeleo.

 

WANACHAMA WA MVIWATA WAANZISHA SACCOS.

Wanachama wa MVIWATA kata ya Magungu wilaya Kiteto mkoani Manyara wameanzisha SACCOS ili kuweza kupata huduma za kifedha. SACCOS hiyo ijulikanayo kama MANGE SACCOS ni muunganiko wa vijiji vitatu Magungu, Nhati na Emarti. SACCOS hiyo imeanzishwa kutokana na uhamasishaji uliofanywa na wananchama kwa kushirikiana na viongozi wa mitandao ya msingi Magungu na Nhati.

Wanachama hawa wa MVIWATA waliamua kuanzisha SACCOS kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ukosefu wa mitaji, umbali wa huduma za kifedha na mikopo ya mabenki yenye riba kubwa. Wanachama hawa wameanzisha SACCOS ili kukuza uchumi na kupunguza umaskini, SACCOS hii itawawezesha wanachama  kuweza kukopa kwa malengo ili kuendesha shughuli zao mbalimbali ikiwemo kilimo na biashara. Kwasasa SACCOS hiyo ina wanachama 70, wanaume 40 na wanawake 30. Mange SACCOS ina mpango wa kufikia wananchama 200 kwa kipindi cha miaka miwili.

Aidha wanachama hao wameshukuru shirika la MVIWATA kwa mchango wake kwa kusaidia katika hatua ya uanzishwaji wa SACCOS ambapo shirika liligharimia wanachama 8 kwenda ziara ya mafunzo  kuhusu SACCOS. Wanachama hao wa MVIWATA walienda katika SACCOS 2 zilizopo mkoani Morogoro, Kinole SACCOS  na Mkuyuni SACCOS. Katika ziara hii ya mafunzo waliweza kujifunza mengi ikiwemo uendeshaji, mafanikio pamoja na changamoto.

SACCOS nyingi zinazoanzisha huwa zinachangamoto kubwa sana na saa nyingine hupelekea kufa kabisa sababu hizi ni kama ukosefu wa uaminifu kwa wanachama wenyewe, ukosefu wa uaminifu kwa wasimamizi na watendaji wa SACCOS kutokuwa na elimu ya kutosha. Suala hili Mange SACCOS wamelitafakari kwa kina na kukubali kuwa watakabiliana na changamoto hizi, wakiifuata kauli mbiu yao isemayo “hakuna kushindwa tukiwa waaminifu, SACCOs ni chombio cha huduma sio chombo cha huruma”.

 

MVIWATA YAENDESHA MAFUNZO YA VIPIMO WILAYA YA KILOSA

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania MVIWATA umeendesha mafunzo ya wakala na vipimo yaliyofanyika katika vijiji vya Mateteni, Msowelo, Kaladasi na Mambegwa wilayani Kilosa mkoani Morogoro. Lengo la mafunzo haya ni kuwafanya wakulima kutambua umuhimu wa kupima mazao yao kwa kutumia vipimo sahihi kabla ya kuyauza, pia kuweza kupata faida ya kile walichokizalisha.

“Leo tutatoa elimu elekezi kuhusiana na vipimo. Tutafundishwa umuhimu wa vipimo halali na baada ya mafunzo haya azimio liwe ni kuuza bila lumbesa”alisema mwezeshaji Ndugu Joseph Sengasenga.

Vipimo ni muhimu sana kwa  wakulima kwani vinawawezesha kuuza mazao yao kwa faida na kwa haki bila dhuluma. Lumbesa imekuwa ni kero kubwa sana kwa wakulima wadogo wilayani Kilosa kwani wamekuwa wakiuza mazao yao kwa ujazo uliozidi kipimo. Hali hii mekuwa ikiwakandamiza wakulima na kuwarudisha nyumba kimaendeleo.

Afisa vipimo kutoka wakala wa vipimo mkoani Morogoro Bi Happy Titi alisema “ Kupima kwa kutumia mzani ni muhimu. Mzani unakusadia kupima uzito sahihi. Dhumuni la vipimo batili ni kumdhulumu mkulima. Inaweza kuwa ngumu kwa mtu kutumia mzani lakini ni muhimu. Inawezekana hamjapata elimu  kwa jinsi wafanyabiashara wanavyowaibia. Kati yenu na wafanyabiashara wanaopata faida ni wafanyabiashara sababu wanawadhulumu kupitia ujazo unaozidi. Leo ntafundisha matumizi ya mizani, wakala wa vipimo kazi yetu ni kuwapa elimu sahihi kuhusu mizani. Huwezi kuzuia  lumbesa kwa macho mizani ni muhimu. Tunataka mazao yote yafungwe kwa mfumo mmoja. Usipozingatia sheria utaibiwa,  mfanyabiashara nia yake ni kumuibia mkulima atengeneze faida”

Sheria za vipimo zilizopo zinaeleza wazi kwamba mazao ya chakula hayaruhusiwi kufungwa kwa ujazo unaozidi. Mazao yote yasizidi kilo mia na yafungwe kwa zipu yaani kusiwe na kilemba kama wengi wanavyoita. Mkulima auze kwa kilo zinazopimwa katika mzani sahihi. Maana kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara wakienda kunua mazao wakiwa na vipimo vyao tayari. Hili ni kosa na hii hairuhisiwi kisheria kwani ni aina ya wizi unaofanywa kwa wakulima.

Aidha Yahya Kagombe kutoka kijiji cha Mateteni anasema “ kwa mfano nimevuna mpunga mfanyabiashara anakuja kununua na anataka kupima kwa debe hakubali mzani na mimi ninahitaji hela kwa muda huo , je nifanyeje. Swali hili lilijibiwa na afisa vipimo Bi. Happy Titi anasema ‘ Suala hili la kuzuia kuuza kwa lumbesa haliwezi kufanikiwa kama hatuna kauli ya pamoja . Mfanyabiashara akiona wewe una shida ndo anatumia huo mwanya. Kama wakulima kwa pamoja mkubaliane kuweka mfumo sahihi kwa kutumia  mizani msikubali kuuza kwenye madebe au vibaba.Tuwe na msimamo wa kukataa vipimo batili. Kwa pamoja tukikataa lumbesa utaratibu wa kutotumia mizani utaisha. Hili lipo mikononi mwenu kulikataa kwa pamoja.’’

Lumbesa imekuwa ikiwaumiza wakulima na kuwafanya kuwa masikini zaidi. Iangaliwe namna ya kutatua changamoto hii kwa pamoja . “ Changamoto kama hii ni muhimu kuwa na soko la pamoja ili kuuza mazao yetu. Tatizo hili linaweza kumalizika tukiwa pamoja. Kwa mtu mmoja mmoja hatuwezi kutatua changamoto hii lakini kwa pamoja tunaweza. Mnapoaandaa mikutano ya kimtandao ni muhimu kuwaalika wenyeviti wa vijiji waje katika kikao ili suala hili liwe katika mpango wa kijiji” anasema Joseph Sengasenga.

 

Aidha wakulima wametaka viongozi wa mtandao waitwe na kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo. Ili waweze kutengenezewa  uelewa na namna ya kujisimamia wenyewe. Matumizi ya lumbesa kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakiwaumiza wakulima kwani wamekuwa wakizalisha kwa gharama kubwa lakini faida wanayoipata hailingani na gharama za uzalishaji.

Wakulima walihimizwa  kuyauza na kuyapima mazao yao kwa mzani ambao umethibitishwa na wakala wa vipimo. “Kumekuwa na tabia  kwa baadhi ya watu tunapoenda kukagua mizani wanakimbia au kujificha kabisa. Kwa pamoja ili kuzuia vipimo batili tuzuie hili. Usitumie mizani ambayo haijathibitishwa na wakala  wa vipimo. Mizani iliyothibitishwa na wakala na vipimo  unakuwa  na stika ya wakala wa vipimo, nembo ya wakala wa vipimo , tarehe, mwezi na mwaka ambayo mzani ulikaguliwa na tarehe mwisho wa matumizi. Hivyo usitumie mzani usiokuwa na alama hizi kwani tukikukamata tutakuchukulia hatua za kisheria” anasema Bi Happy Titi.

Daudi Omary mkazi wa kijiji cha Kaladasi anasema “Kiujumla ziara ni nzuri kwani kuna mambo tulikuwa gizani kwani tulikuwa hatujui kuna kitengo cha mizani elimu hii itatusaidia sana. Elimu kama hii watu wengi hawana kwa sisi tulioipata hapa tunaweza kuwaelimisha na wengine haya tuliyojifunza”

Japokuwa lumbesa hairuhusiwi lakini saa nyingine wakulima wanalazimika kuuza kwa lumbesa kutokana na matatizo wanayokabiliana nayo. Haya yanathibitishwa na bi Elizabeth Muhina ” Haya mafunzo nimeyapokea nimeyaelewa inabidi nikahamasishe na wengine. Tupate soko la uhakika tuepukane na lumbesa. Kwani hali hii inatukandamiza sana. Mfano hapa kwetu kuna kitu kinaitwa gobogobo, mpunga ukishatoa majani kabla hujachanua mfanyabiashara anakupa hela debe moja shilingi 5000/=. Ukishavuna unampa mpunga sasa hapa utaendelea kweli. Inaweza ikatokea kwamba mwaka huo mvua ni chache hivyo hujapata mavuno. Huwezi kurudisha ile hela uliyochukua kwasababu hujauza. Unaishia kupelekwa mahakamani kwasababu ya madeni.. Nafikiri tukipata soko la pamoja kila kitu kitaenda sawa hatutaweza kuwa na gobogobo.

Kupitia mafunzo haya wakulima wametambua umuhimu wa vipimo na kutokubali kuuza mazao yao kwa lumbesa. Ambayo imekuwa inawanyonya  na kuwafanya kuwa maskini siku hadi siku huku wafanyabiashara wakitengeneza faida kubwa.

THE GUARDIAN ARTICLE TITLED ‘’NEW PUSH IN PIPELINE FOR ACCEPTANCE OF GMO SEEDS AFTER SUCCESSFUL TRIALS’’ IS A PROPAGANDA CAMPAIGN

1.We have been shocked by a newspaper article titled ‘’New Push in Pipeline for acceptance of GMO seeds after successful trials “ which was published on the Guardian of 2nd November 2018 claiming that Tanzania Agricultural Research Institute (TARI) has joined farmers across the country in pushing for changes to the existing agricultural laws to allow the use of genetically modified organisms (GMO) seed varieties because they are drought resistant and can’t be easily destroyed by pests including armyworms. Furthermore, the reporting states that “the farmers are also said to have concurred that the use of GMO seeds will ensure bumper harvests while also boosting their own incomes”.

Clearly this article is misleading, unsubstantiated and wants to use farmers as a ploy to convince the public that farmers are in desperate need of GMO seeds which is completely untrue.

2. We are the national farmers’ organisation with members in all regions of Tanzania. We have debated in many forums on GMOs pros and cons and arrived at one conclusion that GMOs are not beneficial to the farmers and to the nation of Tanzania, economically and environmentally. In all our discussions, all of which have been attended by media, farmers have called for our Government not to allow GMOs to be used in the country for obvious reasons that neither farmers nor the nation shall benefit from GMOs. This position of farmers was crystal clear during our recent convergence of at least 2600 farmers which was held in Morogoro, on 5 – 7 October 2018, in Morogoro.

3. We therefore ask the reporter to tell the public which “farmers across the country are pushing for changes to existing agricultural laws to allow the use of genetically modified organisms (GMO) seeds” and which farmers have concurred that “the use of GMO seeds will ensure bumper harvests while also boosting their own incomes”. We challenge the reporter to come up with statistical evidences on these farmers the reporter is referring to especially since this article refers to the work of a scientific body, TARI.

4. Otherwise, the article in the Guardian, as the case is for the article in Mwananchi of 10 November 2018 titled “Mbegu ya Dhahabu: Mbegu za GMO zinavyoweza kuwaepusha Wakulima na Viuatilifu’ once again proves an ongoing media campaign and propaganda to misinform the public and promote GMOs for the interest of multinational companies while disregarding the Tanzanian national interests.

5. During the symposium to mark 3 years of President J.P. Magufuli at University of Dar es Salaam, the President said, when talking about Stigler’s Gorge, that “no one can teach us about environment”. Borrowing these words, certainly, no one can teach the farmers what is good for us and no one else can talk on our behalf, especially on GMOs.

6. We repeat our call to our Government not to allow GMO seeds to be used in our country since no one but multinationals stand to gain at the cost Tanzanian small holder farmers, our economy, our genetic resources and our health.

Download PDF press release

MIAKA 25 YA KUWAUNGANISHA WAKULIMA TANZANIA

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) tumeadhimisha miaka 25 ya kuwaunganisha wakulima. Mgeni Rasmi katika maadhimisho haya alikuwa ni Waziri Mkuu Mhe, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.John Pombe Magufuli.

Maadhimisho haya yalihudhuriwa na wakulima zaidi ya 2000 kutoka sehemu mbalimbali za nchi. Pamoja na hao pia walikuwepo viongozi wa serikali, balozi, mashirika wenza na wageni waalikwa.

ZIARA YA KATIBU MKUU WA CCM DK. BASHIRU ALLY ATEMBELEA OFISI ZA MVIWATA TAIFA MKOANI MOROGORO

Katibu mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally hivi karibuni alitembelea ofisi za MVIWATA Morogoro, kama rafiki zake ambao amekuwa nao mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa mkulima mdogo anakombolewa.

Katika ujio wake aliambatana na viongozi mbalimbali wa chama. Katibu mkuu alipokelewa na watendaji wa MVIWATA na wakulima wakiongozwa na Mwenyekiti na Mkurugenzi wa MVIWATA. Alipata fursa ya kujionea mazao na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na vikundi vya wakulima.

Mwenyekiti Ndugu Abdul Gea alianza ufunguzi wa shughuli kwa kusema“Dr Bashiru kama katibu wa CCM, MVIWATA tumekuwa na mafanikio mengi. Na pia tuna changamoto, tumeshiriki katika ujenzi wa masoko kumi na moja hapa nchini lakini kumekuwa na changamoto katika masoko ya Kibaigwa,Nyandira na Kinole.Kwani mikataba tulioingia na halmashauri imekuwa haisimamiwi ipasavyo.Mengi nitayaeleza hapo baadae lakini sasa naomba nitangaze kuwa shughuli hii imefunguliwa rasmi”.

Baada ya mwenyekiti kufungua shughuli na kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA ndugu Stephen Ruvuga alikuwa na haya ya kusema “Ninashukuru kwa kupata fursa ya kutoa taarifa fupi. Karibu katika makao makuu ya MVIWATA. Ukiwa kama mwanazuoni uliyejipanga kuwasaidia wakulima tunashukuru kwa kuja kututembelea, tunaamini utakuwa nasi na utaendelea kutushika mkono. Siku zote umekuwa mtetezi wa wavuja jasho na wafanyakazi. Kwasababu MVIWATA ni chombo cha wakulima tunaamini kazi yako imepata mtu sahihi”

Aliogeza kuwa “Taasisi yetu inapata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa serikali. Tulipata changamoto ya suala la ujenzi lakini viongozi wa serikali walitusaidia. Tangu mwaka jana tumetekeleza mpango mkakati wa uhakika wa ardhi, uhakika wa soko na uendeshaji wa taasisi”

Mkurugenzi mtendaji pia aligusia changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima ikiwa ni pamoja na ugawaji wa ardhi kwa maeneo yaliyofutwa hati na na muheshimiwa Raisi. Uzalishaji na udhibiti wa mifumo ya kilimo, kwani kilimo cha kisasa kinahitaji sana pembejeo, ambapo alisema inabidi kuwa makini ili kujua ni aina gani ya kilimo tunakitaka ili kufanya uzalishaji kuwa endelevu. Suala la fedha kwaajili ya uendeshaji ni tatizo. Masoko kwa wakulima imekuwa ni shida na tatizo hasa lipo kwenye usambazaji na sio uhitaji. Mipango inayofanyika inazingatia ASDP 2 na utekelezaji wake unaendana na kile kinachofanywa na serikali.

“Taasisi ina mapango wa kufungua redio yake ili kufanya sauti ya mkulima isikike. Pia tuna mpango wa kufungua kiwanda cha uchakataji mazao, tunaamini kuwa siku kutakuwa na kiwanda hicho na kitafanya kazi. Kama ilivyokuwa mwanzo wakati tuanza shirika hili.Tulianza kidogo na kulikuwa na changamoto nyingi lakini sasa tumefika hapa ni kwasababu ya kuishi katika ndoto zetu”Stephen Ruvuga

Aidha alihitimisha kwa kusema kuwa” Changamoto zipo, katibu mkuu ni mtafiti wa ardhi na unaelewa changamoto na sheria za ardhi. Tunaamini kuwa utafiti wako utatusaidia. Tunashukuru kwa kututembelea MVIWATA licha ya majukumu uliyonayo”

Baada ya utangulizi wa Mwenyekiti na Mkurugenzi ukafika wasaa wa mgeni rasmi kutoa yake machache kwa hadhara iliyokuwepo.

“Ninashukuru nipo nyumbani. Mwenyekiti na Mkurugenzi mmesema mazuri kunihusu na ninashukuru. Sifa ziwaendee watanzania kwa kunisomesha kwa kodi zao hatimaye nikaweza kupata shahada zote tatu na siwezi kuwasahau watanzania. Nina deni kubwa la kulipa utumishi uliotukuka. Kazi niliyopewa kuwa mtendaji wa chama kinachoongoza serikali ni jukumu kubwa mno”

Katika maelezo yake katibu mkuu alisema inabidi kufanya tafiti zitakazotatua changamoto za wafanyakazi na wavuja jasho na kutafuta majawabu katika eneo la uzalishaji mali. Kwani katika maeneo hayo kuna mambo ambayo bado hayajafanyiwa kazi ya kutosha. Lazima kuwe na misingi ya kutetea  haki za wanyonge na kusimamia utu.

Katibu mkuu aliongeza kuwa kama taifa bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kulinda wafanyakazi, kwasababu kumekuwa na dhuluma na unyonyaji. Sera ni miongoni mwa vitu vinavyokwaza juhudi za kujiendeleza hasa kwa watu wa kipato cha chini ambao ni wazalishaji wadogo. Ili kuweza kuwa na maendeleo amewataka wakulima kuunda chombo cha kujitetea ili kukata minyororo na mirija ya unyonyaji. Kwani serikali haiwezi kusikiliza mahitaji ya mtu mmoja mmoja hivyo ni lazima wawe na chombo cha kuwapazia sauti.

Nidhamu na uwajibikaji ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya taasisi yoyote “Miaka ishirini na tano imewasaidia sana kupunguza madhila yenu. Vyombo hivi vinapaswa viwe na nidhamu na wa watumishi ni lazima wawajibike ipasavyo. Sio hivyo tu bali viongozi wawe madhubuti katika usimamizi mzuri wa vyombo vyao na wasijiingize katika siasa. Nimedhamiria kupambana na ufisadi na unyonyaji dhidi ya wazalishaji wadogo. Msione haya kupaza sauti kwa kiongozi anayewatetea” Dokta Bashiru.

Ametahadharisha kuwa Afrika inanyemelewa na ukoloni mpya ili kudhibiti rasilimali zake. Hasa ardhi na vilivyomo. Watu wanaoweza kutulinda dhidi ya ukoloni huu ni wakulima wadogo wadogo,ambao ndio watumiaji wakuu wa ardhi. Bado azimio la Arusha lina mashiko mpaka sasa.

Ameiasa taasisi ya MVIWATA kuzingatia mambo mbalimbali katika utendaji wake ikiwemo kuwa chombo kinachowajibika, mtazamo wa kujitegemea, kuwekeza katika rasimali watu, watumishi kujitoa zaidi kwa kufanya kazi zaidi, kuacha uroho na ubinafsi, kuchagua aina ya misaada kutoka kwa wahisani, lazima kujua lengo la muhisani katika msaada anaoutoa na pia kuwalinda wafanyakazi kwa kuwapa maisha ya staha.

Ameeleza kuwa uwepo utaratibu mzuri wa mawasiliano kupitia ofisi ili MVIWATA iwe kama daraja la serikali na wavuja jasho. Mtandao huu upanuke usiwe wa wakulima pekee bali kuwe na mtandao wa wavuvi na wafanyabiashara pia. Amependekeza kuwa katika mkutano mkuu kuwe na mijadala zaidi na sio hotuba ili watu waweze kutoa hoja na mitazamo yao. kama ikiwezekana na wao kama serikali wapate mualiko ili washiriki katika majadiliano hayo.

MVIWATA ni taasisi ya wakulima hivyo wakulima nao walipewa kipaumbele katika kuwasilisha kero zao kwa mgeni rasmi ambapo waliuliza maswali tofauti mengi yakilenga changamoto za ardhi na masoko.

Bi.Arafa Simba kutoka Kilosa aliwasilisha kero kati ya Halmashauri ya Wilaya na wananchi ambao bado hawajakabidhiwa hati za shamba lililogawiwa kutoka kwa mwekezaji na hivyo wao kukosa ardhi ya kufanya shughuli za kilimo. Hivyo kumuomba Katibu Mkuu awasaidie katika suala hili waweze kupata ardhi na kuendelea na shughuli zao.

Richard Hanga kutoka Kilombero alieleza kuwa kumekuwa na mgogoro wa ardhi kati ya kijiji na kampuni ya uzalishaji sukari ya Kilombero Plantation Limited (KPL). Ambapo kampuni hiyo ilifanya utanuzi wa mipaka na kuchukua sehemu ya ardhi ya wanakijiji. Huku wananchi wakibaki bila ardhi, amemuomba katibu mkuu kusaidia kutatua mgogoro huo.

Iddy Ally kutoka wilaya ya Kilosa alitoa changamoto yake kuwa wamezuiliwa kufanya kazi katika eneo ambalo liligawiwa kwa wananchi na kisha likarudishwa kwa mwekezaji. Mpaka sasa hawana ardhi ya kulima na kumekuwa na vitendo vya kinyanyasaji kwa wananchi vinavyofanywa na walinzi wa mwekezaji huyo.

Frolence Haule kutoka Ruvuma alitoa kero yake ya kuwepo kwa wawekezaji wanaohodhi maeneo makubwa. Wamepeleka matatizo yao kwa viongozi wa serikali lakini kumekuwa na mwitikio hasi katika suala lao. Hivyo ameomba serikali itafute mwarobaini wa kero hii kwani wananchi hawana ardhi ya kulima.

Zainabu Kisegere kutoka wilaya ya Kilosa kata ya Msowelo amesema serikali ilirudisha ardhi kwa wananchi lakini wilaya imechukua hiyo ardhi tena na kuigawa kwa wageni. Hivyo anashindwa kuilewa wilaya kwa kushindwa kusimamia ardhi hiyo na kutaka maelezo kutoka kwa katibu.

Bi. Otensia Thomas kutoka Morogoro alitoa kero yake ya baadhi ya watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Morogoro vijijini kuchukua vyanzo vya mapato ya masoko yaliyojengwa na MVIWATA pamoja na unyanyasaji kwa wananchi. Hivyo anaomba serikali iwasaidie kuondokana na kero hii.

Jeremia Maina kutoka Dodoma amemuomba Katibu Mkuu kuwashughulikia watumishi wa serikali wanaosema kuwa wakulima hawana weledi na viongozi ambao ni kero kwa wananchi hali ambayo imesambaratisha na kuvunja umoja wa wakulima wadogo katika kijiji cha Kibaigwa.

Katibu Mkuu alijibu kero hizo kwa kutoa maelezo ya jumla. Alieza kuwa “nawashukuru kwa kuwa wa wazi. Dhana ya uwekezaji wa maana wenye manufaa na unaojenga uchumi wa kitaifa ni ule wenye uhusiano na uzalishaji. Uwekezaji katika Afrika umekuwa wakiporaji. Katika mazingira ya kiafrika mwekezaji ni mkulima. Mwekezaji anayezalisha kwaajIli yake na kutoa ziada katika uchumi ni mkulima. Kama unatafuta sekta halisi katika uchumi wetu ni sekta ya kilimo. Sahau amani kama hutadhibiti rasilimali ya ardhi. Mchakato wa ardhi popote ulipo usimame tujiridhishe kama ushirikishwaji ulitosha. Amekiri kuwa ardhi zilizotwaliwa na Raisi bado zina utata. Ninaomba myaandike haya mliyoyasema kwa vielelezo na ushahidi wenye viambatanisho tutatoa majawabu”

“Kuhusu suala la masoko andikeni barua ipelekwe kwa Waziri wa TAMISEMI. Serikali chini ya Mheshimiwa Raisi haitabadilisha msimamo wa kuwatetea wafanyakazi na wakulima. Niwatie moyo kuwa siku zote tabia ya mtu mnyonyaji ni maneno ya kebehi hivyo msikatishwe tamaa na maneno hayo. Tukigundua unadhalilisha wakulima tutakuchukualia hatua”.

Amehitimisha kwa kuwashukuru wananchi kwa niaba ya Raisi na kusema kuwa pongezi zinazotolewa zinawajenga na kuwafanya waone kuwa wana deni kubwa la kuwalipa watanzania. Na pia amepokea taarifa na mapendekezo yaliyotolewa na kuahidi kuwa serikali itayafanyia kazi ili kutetea maslahi ya wavuja jasho.

NAIBU WAZIRI WA KILIMO MHE. OMARI MGUMBA AFANYA ZIARA YA KIKAZI KATIKA OFISI ZA MVIWATA TAIFA MKOANI MOROGORO.

Naibu Waziri Wa Kilimo Mhe. Omari Mgumba amewataka wakulima kuacha kulima kilimo cha mazoea na badala yake wawatumie wataalamu kutoka mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) pamoja na chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine SUA kwa lengo la kupata ujuzi zaidi kuhusu uzalishaji wa mazao yaliyo bora na yenye tija pamoja na masoko kwa lengo la kujikwamua na wimbi la umasikini.

Haya yanabainshwa na naibu waziri huyo wakati akifanya ziara ya kikazi katika ofisi za Makao Makuu ya Mtandao Wa Vikundi Vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) pamoja na chuo kikuu cha Kilimo cha Sokoine cha SUA Mkoa wa Morogoro, ambapo waziri huyo alijionea shughuli mbalimbali zinafanywa na taasisi hizo ikwemo MVIWATA.

Naibu Waziri Mhe. Mgumba amebainisha malengo ya ziara hiyo katika ofisi hizo za Mtandao Wa Vikundi Vya Wakulima MVIWATA kuwa ni pamoja na kuangalia jinsi mtandao huo wa wakulima unavyotekeleza  mpango mkakati wa kilimo yaani ASDP2,  kujifunza shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na MVIWATA pamoja na kujadiliana changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ya kilimo nchini hasa kwa upande wa wakulima.

Katika kutekeleza mpango mkakati wa kilimo yaani ASDP2, naibu waziri Mgumba ameupongeza Mtandao huo wa vikundi vya wakulima MVIWATA kwa kuweza kufanya shughuli zake kuendana na mpango huo huku pia akisifu utendaji wa mtandao huo kuanzia ngazi ya chini mpaka ya juu.

Niabu waziri ameelezea shughuli za MVIWATA kuwa hazina tofauti sana na Ushirika ambao una malengo ya kuwanufaisha wakulima wadogo hapa nchini kwa kuwawezesha wakulima kupata taarifa sahihi za kilimo na masoko, kuongeza ubora wa mazao na vipimo sahihi pale wanapokuwa wakitaka kuuza mazao yao sehemu mbalimbali nchini.

Kupitia mawasilisho yaliyofanywa na MVIWATA katika ziara hiyo, naibu  waziri wa kilimo Mhe Mgumba amekiri uwepo wa changamto kubwa katika ardhi kwa kuelezea kuwa zaidi ya asilimia 70% ya ardhi yote nchini inamilikiwa na vijiji lakini  Naibu waziri Mgumba anapatwa na hali ya sintofahamu kuhusu umiliki wa ardhi hiyo kwa vijiji kutokana maeneo mengi ya ardhi katika vijiji inamilikiwa na wawekezaji ambao wameshindwa kuendeleza ardhi hiyo hali inayasbabisha ardhi hiyo kuwa mashamba pori.

Katika suala la changamoto la uendeshaji wa masoko yaliyojengwa na MVIWATA katika halmashauri mbalimbali hapa nchini, Mhe naibu waziri Mgumba amekiri uwepo wa upotevu mkubwa fedha ndani ya halmashauri na kusisitiza kuwa mapato yote ya ndani ya halmashauri hayaendi hazina kama inavyobainishwa huku akiahidi kufuatilia fedha zote zilizokubalika kurejeshwa kwenye masoko kwa ajili ya uendeshwaji wa masoko hayo kutokana na sasa

Kabla ya kutembelea ofisi za MVIWATA naibu huyo waziri ametembelea chuo kikuu cha cha Kilimo cha Sokoine SUA kwa lengo la kujionea shughuli mbalimbali za kilimo zinazofanya na chuo hicho, huku akitoa wito kwa taasisi hiyo ya elimu kutoa elimu ya kutosha kwa wakulima kuhusu kilimo cha kisasa na chenye tija kwa lengo la kumnyanyua mkulima kutoka katika wimbi la umasikini kutokana na kulima kilimo cha mazoea.

Mwisho.

MKUTANO MKUU WA DHARURA MVIWATA NGAZI YA KATI KAGERA WAFANYIKA

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) ngazi ya kati Mkoa wa Kagera wafanya mkutano mkuu wa dharura. Mkutano huu umefanyika tarehe 5 Julai 2018 katika ukumbi wa ELCT Hotel Bukoba na ulihudhuriwa na wajumbe 92 (wanawake 37 na wanaume 55) kutoka wilaya za Muleba, Ngara, Kyerwa, Misenyi na Bukoba Vijijini. Mkutano huu umefanyika kwa mujibu wa katiba ya MVIWATA ikiwa na ajenda za Kufungua Mkutano Mkuu wa Dharura, Salamu za Serikali, Kujadili Maendeleo ya MVIWATA Kagera, Kupokea na kujadili taarifa ya ukaguzi wa ndani wa MVIWATA Kagera, Uchaguzi wa kamati ya uongozi na Kufunga Mkutano.

Katika uwakilishi wa serikari Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyerwa Ndugu Greyson Mwengu alitoa nasaha zake kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa ambaye ndiye aliyekuwa mgeni mwalikwa wa mkutano huo lakini hakuweza kufika kutokana na kubanwa na shughuli mbalimbali za serikali.

Ndugu Mwengu kwanza alitoa shukrani kwa kuialika serikali katika mkutano huo. Akitumia kaulimbiu ya mkoa ya “Kazi, Amani na Maendeleo” Ndugu Mwengu alibainisha kwamba kwa kupitia kwa haraka haraka ameona kwamba malengo ya taasisi ya MVIWATA ni mazuri kwani ni ya kuunganisha wakulima kama lilivyo lengo la serikali.  Alieleza kwamba katika mkoa wa Kagera kilimo ni shughuli muhimu sana hasa la zao la kahawa. Aliitaka MVIWATA kujielekeza katika zao la kahawa katika shughuli zake katika mkoa wa Kagera. Amesisitiza ushirikiano katika shughuli za kiuchumi kwa wakulima kwa maslahi ya wakulima na kwa maslahi ya nchi.

Pia ameipongeza MVIWATA kwa kutekeleza kwa vitendo sera za Serikali kwa kuwaunganisha wakulima wadogo katika vikundi na mitandao ili kujipatia maarifa, kubadilishana mawazo na kuwa na sauti ya pamoja katika kutetea maslahi yao kiuchumi na kijamii. Alibainisha azma ya Serikali katika wilaya ya Kyerwa kuiunga mkono MVIWATA katika jitihada za kuwaendeleza wakulima.

Katika mkutano huo kulikua na majadiliano kuhusu maendeleo ya  MVIWATA katika Mkoa wa Kagera ambao ulianza kwa maelezo mafupi ya historia ya MVIWATA –Kagera tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004 mpaka sasa, mafanikio, changamoto na jitihada ambazo MVIWATA Taifa ilifanya ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizojitokeza ndani ya MVIWATA ngazi ya kati Kagera. Maelezo hayo yalitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA, Ndugu Stephen Ruvuga.

Baada ya majadaliano, wajumbe walieleza kusikitishwa na mwenendo wa viongozi wa tawi la MVIWATA-Kagera kwa kuchochea migogoro na migawanyiko katika taasisi na kutowaheshimu wanachama.  Wajumbe pia walijadili kukiukwa wazi misingi na maadili ya MVIWATA hivyo kuazimiwa kuvuliwa uanachama kwa baadhi ya viongozi.

Vilevile Wajumbe wa mkutano huo waliazimia Ofisi za MVIWATA ngazi ya kati Kagera zihamishiwe katika Mji wa Bukoka kutoka Muleba ili ziweze kuwa karibu zaidi na wanachama walio katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kagera kutokana na mazingira ya Kijiographia ya Mkoa huo. Azimio hilo lilikuja baada ya wajumbe kupiga kura ya kukubali kuhamisha ofisi hizo.

Vile vile Mkutano huo wa dharura ulifanya Uchaguzi wa viongozi wapya wa MVIWATA ngazi ya kati Kagera ambapo wajumbe tisa wa kamati ya uongozi walichaguliwa kutoka wilaya nne za Mkoa huo, Wilaya hizo ni Muleba, Ngara, Bukoba Vijijini na Kyerwa. Baada ya safu kukamilika wajumbe wa kamati mpya ya uongozi walikaa ili kuchagua viongozi wa Kamati ya Uongozi  ambao ni  Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Mtunza Hazina. Hatimaye, uchaguzi ulikamilika ambapo safu kamili ya uongozi wa MVIWATA Kagera ilipatikana kama ifuatavyo;

  1. Josias Kagoma                                   Mwenyekiti
  2. Selemani Sadiki                                 Makamu Mwenyekiti
  3. Abadini Rwakibanda                       Katibu
  4. Jirian Rajabu                                       Mweka Hazina
  5. Adelina Meshack                             Mjumbe
  6. Grace Bitegeko                                 Mjumbe
  7. Prosper Mukiza                                Mjumbe
  8. Mariagorethi Gabriel                      Mjumbe
  9. Teddy Innocent                                Mjumbe

MWISHO.

 

MVIWATA YAENDESHA KIKAO CHA MASHAURIANO KATI YA WAKULIMA NA WATAFITI NCHINI

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) wamefanya kikao cha mashauriano kati ya wakulima na watafiti wa kilimo ili kupata namna bora ya kuwahusisha wakulima katika kutoa vipaumbele vya tafiti mbalimbali za kilimo zinazoendelea hapa nchini. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Andrew Hepelwa uliopo katika ofisi za MVIWATA Makao Makuu mkoani Morogoro.

Kikao hicho kilihusisha watafiti kutoka kanda saba za kitafiti hapa nchini zinazosimamiwa na Taasisi ya Utafiti wa kilimo nchini TARI (Tanzania Agriculture Research Institute). Kanda hizo ni, Kaskazini (Selian), Kusini (Naliendele), Kanda juu Kusini (Uyole), Kanda ya Mashariki (Ilonga), Kanda ya kati (Makutopora), Kanda ya ziwa (Ukiriguru) na Kanda ya magharibi (Tumbi).

Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA Ndg. Stephen Ruvuga alieleza kwa ufupi ushiriki wa MVIWATA katika kuhakikisha mkulima mdogo anapata haki anazostahili katika shughuli zake. Vilevile alitoa ufafanuzi wa shughuli zinazofanywa na MVIWATA ikiwa ni pamoja na ujenzi na usimamizi wa miundombinu katika masoko, Umiliki wa Ardhi kama utoaji wa hati miliki za kimila za ardhi, Uanzishwaji wa vyombo vya kifedha mfano SACCOS, Utoaji wa mafunzo ya n kilimo endelevu ili kuongeza ujuzi kwa wakulima wadogo na kuwawakilisha wakulima katika ngazi mbalimbali za majadiliano.

Ndugu Ruvuga alitoa salamu za pongezi kwa Dr. Geoffrey Mkamilo kwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI). Dr. Geoffrey Mkamilo alikuwa mgeni rasmi wa Kikao hicho.

Mkurugenzi wa TARI alieleza muundo wa kiutawala wa taasisi hiyo ambayo ipo kwenye mchakato wa kuundwa katika wizara ya kilimo. TARI ni taasisi itakayoundwa na bodi wa wakurugenzi yenye wajumbe tisa wenye mamlaka ya kuajiri na kuiendesha taasisi hiyo. Shughuli zingine zipo chini ya mkurugenzi wa tafiti za kilimo nchini akishirikiana na wakurugenzi wa vituo mbalimbali vya kitafiti hapa nchini vilivyo chini ya usimamizi wa TARI.

Dr. Mkamilo pia alitoa historia fupi ya tafiti za kilimo hapa nchini kabla na baada ya uhuru. Kabla ya uhuru tafiti za kilimo zilifanyika chini ya utawala wa wajerumani na waingereza ambao ndio waliokuwa watawala wa kipindi hicho na ulilenga mazao ya biashara ambayo yalikuwa ni mali ghafi katika viwanda vya nchi zao.

Baada ya uhuru tafiti zileendelea kufanywa kwa kurithi na kuendeleza tafiti za mazao ya biashara kama ambavyo zilikua zikifanywa na wakoloni. Kwa kipindi hicho kulikua na kituo kimoja kikubwa ambacho kilikua katika mkoa wa Tanga (Amani) ambacho kilianzishwa karne ya 19 na ndio kituo kikongwe zaidi hapa nchini. Baada ya kuongezeka kwa mahitaji ya chakula na serikali kutumia fedha nyingi kuagiza chakula toka nje ya nchi, serikali iliamua kuanza kufanya utafiti wa mazao ya chakula na biashara kwa ujumla. Baada ya tafiti hizo kufanywa mbegu nyingi za mazao ya chakula ziligawiwa kwa wakulima ili waweze kuzalisha mazao ya chakula ya kutosheleza nchi nzima.

Mwaka 1982 serikali ilianzisha taasisi za utafiti zinazohusika na kilimo (TAO) na mifugo (TALIRO) ambapo kufikia mwaka 1989 zilikufa kwa sababu mbalimbali. Katika kuleta mbinu mpya za kufanya tafiti ambazo zitagusa sehemu mbalimbali za nchi, serikali iliamua kuzigawanya kikanda na tangu mwaka 1990 mpaka sasa tafiti zote za kilimo zinafanywa kwa kila kanda na kwa mazao husika yanayopatikana katika kanda hizo.

Katika kikao hicho wajumbe walihoji ushiriki wa wakulima katika kutoa vipaumbele vya tafiti za kilimo hapa nchini katika taasisi mpya ya TARI.  Wajumbe pia walihoji ujuzi wa wakulima wadogo katika kupambana dhidi ya baadhi ya magonjwa ya mazao ya kilimo unazingatiwaje na watafiti katika muundo wa taasisi ya TARI.

Akijibu maswali hayo Dr. Mkamilo alisema katika mfumo mpya wa TARI wakulima watahusishwa katika kuchangia vipaumbele vya tafiti wakiwa ndani ya halmashauri zao ambapo vituo vya kitafiti vinapatikana. Pia aliongeza kuwa watafiti huchunguza baadhi ya njia za asili zinazotumiwa na wakulima katika kukabiliana na magonjwa ya kilimo na kuzipitisha zitumike punde tu wanaporidhia kuwa hazina madhara kwa mmea wenyewe na mtumiaji. TARI itaruhusu utafiti ufanyike baada ya kutambua changamoto za wakulima katika kilimo na kuelewa utafiti huo utawezaje kutatua changamoto hizo na athari za utafiti huo.

Dr Kamilo pia aliongezea kwa kusema TARI itafanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kilimo kama vyuo vikuu kutoka ndani na nje ya nchi baadhi ya vyuo hivyo ni SUA kilichopo mjini Morogoro na kutoka nje ya nchi ni Makerere (Uganda), pia halmashauri mbali mbali za miji na majiji, taasisi mbalimbali za kilimo hapa nchini.

Watafiti kutoka vituo vya kilimo hapa nchini vilivyo chini ya usimamizi wa TARI kwa pamoja walimuomba Mkurugenzi wa MVIWATA kuwahamasisha wakulima ambao ni wanachama wa mtandao huo kushirikiana na watafiti waliopo ndani ya vituo hivyo ili kuwezesha tafiti zenye mafanikio na tija kwa wakulima hapa nchini.

Mwisho Dr. Mkamilo aliishukuru MVIWATA kwa kuwezesha kikao hicho cha mashauriano ambayo yaliwezesha wadau kuelewa majukumu ya TARI na kusaidia watafiti kupata mawazo mapya ya namna bora ya kuwahusisha wakulima katika kutoa vipaumbele vya tafiti za kilimo.

Ndg. Ruvuga alihitimisha kwa kuwashukuru washiriki wote waalikwa kuweza kufika katika majadiliano yaliyofanyika vizuri na kubadilishana uzoefu mbalimbali wa kufanya tafiti za kilimo.

MWISHO.

 

SEMINA YA MIMEA ILIYOBADILISHWA VINASABA (GMO) KWA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE LA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI.

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) umeendesha semina iliyokua na lengo la kutoa elimu juu ya mimea iliyobadilishwa vinasaba (GMO’s) kwa wabunge wa kamati ya kilimo, mifugo na maji pamoja wenyeviti wa kamati za kudumu za bunge za bajeti, biashara na miundominu. Pia kulikuwa na wadau kutoka taasisi za kilimo za serikali na zisizo za serikali pamoja na wakulima katika semina hiyo iliyofanyika mjini, Morogoro.


Akiwakaribisha katika semina hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA Ndg, Stephen Ruvuga alimshukuru Mhe. Spika Ndg, Job Ndugai kwa kuwapa fursa wabunge kuhudhuria katika semina hiyo na kuwataka washiriki kutoa michango yao na uzoefu wao juu ya mimea iliyobadilishwa vinasaba ili kujenga uelewa mpana hivyo kuwasaidia wabunge kutoa maamuzi yatakayoleta tija kwa wakulima nchini.


Semina hiyo ilihusisha watoa mada mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Kutoka ndani ya nchi kulikuwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) iliyowakilishwa na Dr. Nyange, Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) iliwakilishwa na Dr, Patrick Ngwediagi, Kituo cha Utafiti wa Mazao ya Kilimo cha Mikocheni (MARI) iliyowakilishwa na Ndg, Joseph Ndunguru, Dr. Richard Mbunda kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam na kutoka nje ya nchi alikuwepo Dr. Angelica Hilberck kutoka Kituo cha Tafiti za Kibaiolojia, Zurich Switzerland.


Wataalamu hao walielezea mitazamo yao mbalimbali juu ya mimea iliyobadilishwa vinasaba ambapo wawakilishi kutoka COSTECH, TOSCI na MARI walieleza kuwa mimea hiyo ni njia muafaka ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na yenye tija kwa mkulima mdogo katika uzalishaji wake kutokana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa nchini.


Dr. Mbunda alieleza kuwa mimea iliyobadilishwa vinasaba sio chaguo sahihi kwa uhuru na usalama wa chakula. Vilevile tafiti zinaonesha kuwa vyakula vya mimea hiyo havina ladha nzuri kulinganisha na vyakula vinavyotokana na mbegu za asili. Mtaalamu huyo alisisitiza kuwa mimea hiyo itajenga utegemezi wa pembejeo za kilimo (mbolea, mbegu na madawa) kutoka kwa makampuni makubwa ya kibepari.


Dr. Angelica alielezea dhana na chimbuko la GMO na kusisitiza kuwa tafiti zinaonesha kuwa hakuna uhusiano kati ya matumizi ya GMO na ongezeko la uzalishaji wa mazao ukilinganisha na mbegu za asili. Pia alieleza kuwa nchi nyingi za bara la Ulaya zimepiga marufuku matumizi ya GMO na kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya kemikali katika kilimo.


Katika kuhitimisha Ndg. Ruvuga alitoa shukrani kwa wabunge na wadau waliojitokeza katika semina hiyo wakiwemo wakulima na taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali zilizohusika katika kutoa elimu na kujenga uelewa zaidi juu ya mimea iliyobadilishwa vinasaba ambayo imekua ikipokelewa kwa hisia tofauti tofauti na wadau wa kilimo nchini.


Akifunga semina hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Mgimwa alliyekuwa mwenyekiti wa semina hiyo kwa niaba ya wabunge alitoa shukrani kwa MVIWATA kwa kuwezesha semina hiyo kwa sababu imewaongezea uelewa mkubwa juu ya mimea iliyobadilishwa vinasaba. Pia aliomba semina hizo ziwe endelevu ili kundelea kuwajengea uelewa zaidi na hivyo kutoa maamuzi yatakayo leta tija kwa wakulima wadogo nchini.

MWISHO.

NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS (TAMISEMI) MHE, JOSEPHAT S. KANDEGE ATEMBELEA OFISI ZA MAKAO MAKUU YA MVIWATA MOROGORO.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe, Josephat Sinkamba Kandege mapema hii leo tarehe 2 May 2018 ametembelea ofisi za MVIWATA taifa zilizopo katika mtaa wa Bigwa Mkoani Morogoro.

Katika ziara hiyo Mhe, Naibu Waziri amepokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA Ndg Stephen Ruvuga pamoja na wafanyakazi na kufahamishwa shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na MVIWATA nchini ikiwemo ushiriki wa MVIWATA katika ujenzi wa masoko mbalimbali nchini ya wakulima ikiwemo soko la kimataifa la Kibaigwa ambalo hivi karibuni limekuwa na changamoto mbalimbali za kiusimamizi.

Mhe, Naibu Waziri amefurahi kufika katika ofisi za MVIWATA na kuishauri kutumia vyema vikundi vya wakulima katika kuwatafutia wakulima masoko ya mazao yao “ni rahisi sana wanunuzi kununua mazao ya wakulima wakiwa katika vikundi na hiyo inawapa fursa wanunuzi kuwa na uhakika wa mazao wanayoyanunua” alisema Mhe, Josephat Kandege.

Awali kabla ya kufika katika ofisi za MVIWATA Mhe, Josephat Kandege amekiri kuwa amekuwa akiisikia tu MVIWATA na hivyo kuamua kuitembelea na kujionea mwenyewe, “wanasema seeing is believing (kuona ni kuamini) nashukuru sana nimefika hapa leo na kujionea kazi kubwa mnazofanya, hongereni sana” alisema Mhe Naibu Waziri.

Pia ameihakikishia MVIWATA ushirikiano katika masuala mbalimbali na hivyo kuahidi kuitembelea mara kwa mara “naomba niwahakikishie kuwa tupo pamoja, na hivi karibuni nina ziara ya kwenda Matombo, hivyo nitapita hapa niende nanyi ili nipate fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo mnayotekeleza shughuli zenu za kilimo na kujionea mwenyewe shughuli za vikundi vya wakulima huko vijijini”.

Baada ya hapo Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA alimshukuru sana Mhe, Naibu Waziri Josephat S. Kandege kwa kuitembelea MVIWATA na kumuahidi ushirikiano zaidi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

MWISHO.