MVIWATA YAENDESHA KIKAO CHA MASHAURIANO KATI YA WAKULIMA NA WATAFITI NCHINI

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) wamefanya kikao cha mashauriano kati ya wakulima na watafiti wa kilimo ili kupata namna bora ya kuwahusisha wakulima katika kutoa vipaumbele vya tafiti mbalimbali za kilimo zinazoendelea hapa nchini. Kikao hicho kimefanyika katika ukumbi wa Andrew Hepelwa uliopo katika ofisi za MVIWATA Makao Makuu mkoani Morogoro.

Kikao hicho kilihusisha watafiti kutoka kanda saba za kitafiti hapa nchini zinazosimamiwa na Taasisi ya Utafiti wa kilimo nchini TARI (Tanzania Agriculture Research Institute). Kanda hizo ni, Kaskazini (Selian), Kusini (Naliendele), Kanda juu Kusini (Uyole), Kanda ya Mashariki (Ilonga), Kanda ya kati (Makutopora), Kanda ya ziwa (Ukiriguru) na Kanda ya magharibi (Tumbi).

Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA Ndg. Stephen Ruvuga alieleza kwa ufupi ushiriki wa MVIWATA katika kuhakikisha mkulima mdogo anapata haki anazostahili katika shughuli zake. Vilevile alitoa ufafanuzi wa shughuli zinazofanywa na MVIWATA ikiwa ni pamoja na ujenzi na usimamizi wa miundombinu katika masoko, Umiliki wa Ardhi kama utoaji wa hati miliki za kimila za ardhi, Uanzishwaji wa vyombo vya kifedha mfano SACCOS, Utoaji wa mafunzo ya n kilimo endelevu ili kuongeza ujuzi kwa wakulima wadogo na kuwawakilisha wakulima katika ngazi mbalimbali za majadiliano.

Ndugu Ruvuga alitoa salamu za pongezi kwa Dr. Geoffrey Mkamilo kwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI). Dr. Geoffrey Mkamilo alikuwa mgeni rasmi wa Kikao hicho.

Mkurugenzi wa TARI alieleza muundo wa kiutawala wa taasisi hiyo ambayo ipo kwenye mchakato wa kuundwa katika wizara ya kilimo. TARI ni taasisi itakayoundwa na bodi wa wakurugenzi yenye wajumbe tisa wenye mamlaka ya kuajiri na kuiendesha taasisi hiyo. Shughuli zingine zipo chini ya mkurugenzi wa tafiti za kilimo nchini akishirikiana na wakurugenzi wa vituo mbalimbali vya kitafiti hapa nchini vilivyo chini ya usimamizi wa TARI.

Dr. Mkamilo pia alitoa historia fupi ya tafiti za kilimo hapa nchini kabla na baada ya uhuru. Kabla ya uhuru tafiti za kilimo zilifanyika chini ya utawala wa wajerumani na waingereza ambao ndio waliokuwa watawala wa kipindi hicho na ulilenga mazao ya biashara ambayo yalikuwa ni mali ghafi katika viwanda vya nchi zao.

Baada ya uhuru tafiti zileendelea kufanywa kwa kurithi na kuendeleza tafiti za mazao ya biashara kama ambavyo zilikua zikifanywa na wakoloni. Kwa kipindi hicho kulikua na kituo kimoja kikubwa ambacho kilikua katika mkoa wa Tanga (Amani) ambacho kilianzishwa karne ya 19 na ndio kituo kikongwe zaidi hapa nchini. Baada ya kuongezeka kwa mahitaji ya chakula na serikali kutumia fedha nyingi kuagiza chakula toka nje ya nchi, serikali iliamua kuanza kufanya utafiti wa mazao ya chakula na biashara kwa ujumla. Baada ya tafiti hizo kufanywa mbegu nyingi za mazao ya chakula ziligawiwa kwa wakulima ili waweze kuzalisha mazao ya chakula ya kutosheleza nchi nzima.

Mwaka 1982 serikali ilianzisha taasisi za utafiti zinazohusika na kilimo (TAO) na mifugo (TALIRO) ambapo kufikia mwaka 1989 zilikufa kwa sababu mbalimbali. Katika kuleta mbinu mpya za kufanya tafiti ambazo zitagusa sehemu mbalimbali za nchi, serikali iliamua kuzigawanya kikanda na tangu mwaka 1990 mpaka sasa tafiti zote za kilimo zinafanywa kwa kila kanda na kwa mazao husika yanayopatikana katika kanda hizo.

Katika kikao hicho wajumbe walihoji ushiriki wa wakulima katika kutoa vipaumbele vya tafiti za kilimo hapa nchini katika taasisi mpya ya TARI.  Wajumbe pia walihoji ujuzi wa wakulima wadogo katika kupambana dhidi ya baadhi ya magonjwa ya mazao ya kilimo unazingatiwaje na watafiti katika muundo wa taasisi ya TARI.

Akijibu maswali hayo Dr. Mkamilo alisema katika mfumo mpya wa TARI wakulima watahusishwa katika kuchangia vipaumbele vya tafiti wakiwa ndani ya halmashauri zao ambapo vituo vya kitafiti vinapatikana. Pia aliongeza kuwa watafiti huchunguza baadhi ya njia za asili zinazotumiwa na wakulima katika kukabiliana na magonjwa ya kilimo na kuzipitisha zitumike punde tu wanaporidhia kuwa hazina madhara kwa mmea wenyewe na mtumiaji. TARI itaruhusu utafiti ufanyike baada ya kutambua changamoto za wakulima katika kilimo na kuelewa utafiti huo utawezaje kutatua changamoto hizo na athari za utafiti huo.

Dr Kamilo pia aliongezea kwa kusema TARI itafanya kazi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa kilimo kama vyuo vikuu kutoka ndani na nje ya nchi baadhi ya vyuo hivyo ni SUA kilichopo mjini Morogoro na kutoka nje ya nchi ni Makerere (Uganda), pia halmashauri mbali mbali za miji na majiji, taasisi mbalimbali za kilimo hapa nchini.

Watafiti kutoka vituo vya kilimo hapa nchini vilivyo chini ya usimamizi wa TARI kwa pamoja walimuomba Mkurugenzi wa MVIWATA kuwahamasisha wakulima ambao ni wanachama wa mtandao huo kushirikiana na watafiti waliopo ndani ya vituo hivyo ili kuwezesha tafiti zenye mafanikio na tija kwa wakulima hapa nchini.

Mwisho Dr. Mkamilo aliishukuru MVIWATA kwa kuwezesha kikao hicho cha mashauriano ambayo yaliwezesha wadau kuelewa majukumu ya TARI na kusaidia watafiti kupata mawazo mapya ya namna bora ya kuwahusisha wakulima katika kutoa vipaumbele vya tafiti za kilimo.

Ndg. Ruvuga alihitimisha kwa kuwashukuru washiriki wote waalikwa kuweza kufika katika majadiliano yaliyofanyika vizuri na kubadilishana uzoefu mbalimbali wa kufanya tafiti za kilimo.

MWISHO.

 

Mviwata on Facebook

Subscribe to our monthly newsletter