Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania MVIWATA umeendesha mafunzo ya wakala na vipimo yaliyofanyika katika vijiji vya Mateteni, Msowelo, Kaladasi na Mambegwa wilayani Kilosa mkoani Morogoro. Lengo la mafunzo haya ni kuwafanya wakulima kutambua umuhimu wa kupima mazao yao kwa kutumia vipimo sahihi kabla ya kuyauza, pia kuweza kupata faida ya kile walichokizalisha.
“Leo tutatoa elimu elekezi kuhusiana na vipimo. Tutafundishwa umuhimu wa vipimo halali na baada ya mafunzo haya azimio liwe ni kuuza bila lumbesa”alisema mwezeshaji Ndugu Joseph Sengasenga.
Vipimo ni muhimu sana kwa wakulima kwani vinawawezesha kuuza mazao yao kwa faida na kwa haki bila dhuluma. Lumbesa imekuwa ni kero kubwa sana kwa wakulima wadogo wilayani Kilosa kwani wamekuwa wakiuza mazao yao kwa ujazo uliozidi kipimo. Hali hii mekuwa ikiwakandamiza wakulima na kuwarudisha nyumba kimaendeleo.
Afisa vipimo kutoka wakala wa vipimo mkoani Morogoro Bi Happy Titi alisema “ Kupima kwa kutumia mzani ni muhimu. Mzani unakusadia kupima uzito sahihi. Dhumuni la vipimo batili ni kumdhulumu mkulima. Inaweza kuwa ngumu kwa mtu kutumia mzani lakini ni muhimu. Inawezekana hamjapata elimu kwa jinsi wafanyabiashara wanavyowaibia. Kati yenu na wafanyabiashara wanaopata faida ni wafanyabiashara sababu wanawadhulumu kupitia ujazo unaozidi. Leo ntafundisha matumizi ya mizani, wakala wa vipimo kazi yetu ni kuwapa elimu sahihi kuhusu mizani. Huwezi kuzuia lumbesa kwa macho mizani ni muhimu. Tunataka mazao yote yafungwe kwa mfumo mmoja. Usipozingatia sheria utaibiwa, mfanyabiashara nia yake ni kumuibia mkulima atengeneze faida”
Sheria za vipimo zilizopo zinaeleza wazi kwamba mazao ya chakula hayaruhusiwi kufungwa kwa ujazo unaozidi. Mazao yote yasizidi kilo mia na yafungwe kwa zipu yaani kusiwe na kilemba kama wengi wanavyoita. Mkulima auze kwa kilo zinazopimwa katika mzani sahihi. Maana kumekuwa na baadhi ya wafanyabiashara wakienda kunua mazao wakiwa na vipimo vyao tayari. Hili ni kosa na hii hairuhisiwi kisheria kwani ni aina ya wizi unaofanywa kwa wakulima.
Aidha Yahya Kagombe kutoka kijiji cha Mateteni anasema “ kwa mfano nimevuna mpunga mfanyabiashara anakuja kununua na anataka kupima kwa debe hakubali mzani na mimi ninahitaji hela kwa muda huo , je nifanyeje. Swali hili lilijibiwa na afisa vipimo Bi. Happy Titi anasema ‘ Suala hili la kuzuia kuuza kwa lumbesa haliwezi kufanikiwa kama hatuna kauli ya pamoja . Mfanyabiashara akiona wewe una shida ndo anatumia huo mwanya. Kama wakulima kwa pamoja mkubaliane kuweka mfumo sahihi kwa kutumia mizani msikubali kuuza kwenye madebe au vibaba.Tuwe na msimamo wa kukataa vipimo batili. Kwa pamoja tukikataa lumbesa utaratibu wa kutotumia mizani utaisha. Hili lipo mikononi mwenu kulikataa kwa pamoja.’’
Lumbesa imekuwa ikiwaumiza wakulima na kuwafanya kuwa masikini zaidi. Iangaliwe namna ya kutatua changamoto hii kwa pamoja . “ Changamoto kama hii ni muhimu kuwa na soko la pamoja ili kuuza mazao yetu. Tatizo hili linaweza kumalizika tukiwa pamoja. Kwa mtu mmoja mmoja hatuwezi kutatua changamoto hii lakini kwa pamoja tunaweza. Mnapoaandaa mikutano ya kimtandao ni muhimu kuwaalika wenyeviti wa vijiji waje katika kikao ili suala hili liwe katika mpango wa kijiji” anasema Joseph Sengasenga.
Aidha wakulima wametaka viongozi wa mtandao waitwe na kupewa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia vipimo. Ili waweze kutengenezewa uelewa na namna ya kujisimamia wenyewe. Matumizi ya lumbesa kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakiwaumiza wakulima kwani wamekuwa wakizalisha kwa gharama kubwa lakini faida wanayoipata hailingani na gharama za uzalishaji.
Wakulima walihimizwa kuyauza na kuyapima mazao yao kwa mzani ambao umethibitishwa na wakala wa vipimo. “Kumekuwa na tabia kwa baadhi ya watu tunapoenda kukagua mizani wanakimbia au kujificha kabisa. Kwa pamoja ili kuzuia vipimo batili tuzuie hili. Usitumie mizani ambayo haijathibitishwa na wakala wa vipimo. Mizani iliyothibitishwa na wakala na vipimo unakuwa na stika ya wakala wa vipimo, nembo ya wakala wa vipimo , tarehe, mwezi na mwaka ambayo mzani ulikaguliwa na tarehe mwisho wa matumizi. Hivyo usitumie mzani usiokuwa na alama hizi kwani tukikukamata tutakuchukulia hatua za kisheria” anasema Bi Happy Titi.
Daudi Omary mkazi wa kijiji cha Kaladasi anasema “Kiujumla ziara ni nzuri kwani kuna mambo tulikuwa gizani kwani tulikuwa hatujui kuna kitengo cha mizani elimu hii itatusaidia sana. Elimu kama hii watu wengi hawana kwa sisi tulioipata hapa tunaweza kuwaelimisha na wengine haya tuliyojifunza”
Japokuwa lumbesa hairuhusiwi lakini saa nyingine wakulima wanalazimika kuuza kwa lumbesa kutokana na matatizo wanayokabiliana nayo. Haya yanathibitishwa na bi Elizabeth Muhina ” Haya mafunzo nimeyapokea nimeyaelewa inabidi nikahamasishe na wengine. Tupate soko la uhakika tuepukane na lumbesa. Kwani hali hii inatukandamiza sana. Mfano hapa kwetu kuna kitu kinaitwa gobogobo, mpunga ukishatoa majani kabla hujachanua mfanyabiashara anakupa hela debe moja shilingi 5000/=. Ukishavuna unampa mpunga sasa hapa utaendelea kweli. Inaweza ikatokea kwamba mwaka huo mvua ni chache hivyo hujapata mavuno. Huwezi kurudisha ile hela uliyochukua kwasababu hujauza. Unaishia kupelekwa mahakamani kwasababu ya madeni.. Nafikiri tukipata soko la pamoja kila kitu kitaenda sawa hatutaweza kuwa na gobogobo.
Kupitia mafunzo haya wakulima wametambua umuhimu wa vipimo na kutokubali kuuza mazao yao kwa lumbesa. Ambayo imekuwa inawanyonya na kuwafanya kuwa maskini siku hadi siku huku wafanyabiashara wakitengeneza faida kubwa.





