NAIBU WAZIRI OFISI YA RAIS (TAMISEMI) MHE, JOSEPHAT S. KANDEGE ATEMBELEA OFISI ZA MAKAO MAKUU YA MVIWATA MOROGORO.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe, Josephat Sinkamba Kandege mapema hii leo tarehe 2 May 2018 ametembelea ofisi za MVIWATA taifa zilizopo katika mtaa wa Bigwa Mkoani Morogoro.

Katika ziara hiyo Mhe, Naibu Waziri amepokelewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA Ndg Stephen Ruvuga pamoja na wafanyakazi na kufahamishwa shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na MVIWATA nchini ikiwemo ushiriki wa MVIWATA katika ujenzi wa masoko mbalimbali nchini ya wakulima ikiwemo soko la kimataifa la Kibaigwa ambalo hivi karibuni limekuwa na changamoto mbalimbali za kiusimamizi.

Mhe, Naibu Waziri amefurahi kufika katika ofisi za MVIWATA na kuishauri kutumia vyema vikundi vya wakulima katika kuwatafutia wakulima masoko ya mazao yao “ni rahisi sana wanunuzi kununua mazao ya wakulima wakiwa katika vikundi na hiyo inawapa fursa wanunuzi kuwa na uhakika wa mazao wanayoyanunua” alisema Mhe, Josephat Kandege.

Awali kabla ya kufika katika ofisi za MVIWATA Mhe, Josephat Kandege amekiri kuwa amekuwa akiisikia tu MVIWATA na hivyo kuamua kuitembelea na kujionea mwenyewe, “wanasema seeing is believing (kuona ni kuamini) nashukuru sana nimefika hapa leo na kujionea kazi kubwa mnazofanya, hongereni sana” alisema Mhe Naibu Waziri.

Pia ameihakikishia MVIWATA ushirikiano katika masuala mbalimbali na hivyo kuahidi kuitembelea mara kwa mara “naomba niwahakikishie kuwa tupo pamoja, na hivi karibuni nina ziara ya kwenda Matombo, hivyo nitapita hapa niende nanyi ili nipate fursa ya kutembelea baadhi ya maeneo mnayotekeleza shughuli zenu za kilimo na kujionea mwenyewe shughuli za vikundi vya wakulima huko vijijini”.

Baada ya hapo Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA alimshukuru sana Mhe, Naibu Waziri Josephat S. Kandege kwa kuitembelea MVIWATA na kumuahidi ushirikiano zaidi katika utekelezaji wa majukumu mbalimbali.

MWISHO.

Mviwata on Facebook

Subscribe to our monthly newsletter