ZIARA YA KATIBU MKUU WA CCM DK. BASHIRU ALLY ATEMBELEA OFISI ZA MVIWATA TAIFA MKOANI MOROGORO

Katibu mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally hivi karibuni alitembelea ofisi za MVIWATA Morogoro, kama rafiki zake ambao amekuwa nao mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa mkulima mdogo anakombolewa.

Katika ujio wake aliambatana na viongozi mbalimbali wa chama. Katibu mkuu alipokelewa na watendaji wa MVIWATA na wakulima wakiongozwa na Mwenyekiti na Mkurugenzi wa MVIWATA. Alipata fursa ya kujionea mazao na bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na vikundi vya wakulima.

Mwenyekiti Ndugu Abdul Gea alianza ufunguzi wa shughuli kwa kusema“Dr Bashiru kama katibu wa CCM, MVIWATA tumekuwa na mafanikio mengi. Na pia tuna changamoto, tumeshiriki katika ujenzi wa masoko kumi na moja hapa nchini lakini kumekuwa na changamoto katika masoko ya Kibaigwa,Nyandira na Kinole.Kwani mikataba tulioingia na halmashauri imekuwa haisimamiwi ipasavyo.Mengi nitayaeleza hapo baadae lakini sasa naomba nitangaze kuwa shughuli hii imefunguliwa rasmi”.

Baada ya mwenyekiti kufungua shughuli na kumkaribisha mgeni rasmi, Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA ndugu Stephen Ruvuga alikuwa na haya ya kusema “Ninashukuru kwa kupata fursa ya kutoa taarifa fupi. Karibu katika makao makuu ya MVIWATA. Ukiwa kama mwanazuoni uliyejipanga kuwasaidia wakulima tunashukuru kwa kuja kututembelea, tunaamini utakuwa nasi na utaendelea kutushika mkono. Siku zote umekuwa mtetezi wa wavuja jasho na wafanyakazi. Kwasababu MVIWATA ni chombo cha wakulima tunaamini kazi yako imepata mtu sahihi”

Aliogeza kuwa “Taasisi yetu inapata ushirikiano mzuri kutoka kwa viongozi wa serikali. Tulipata changamoto ya suala la ujenzi lakini viongozi wa serikali walitusaidia. Tangu mwaka jana tumetekeleza mpango mkakati wa uhakika wa ardhi, uhakika wa soko na uendeshaji wa taasisi”

Mkurugenzi mtendaji pia aligusia changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima ikiwa ni pamoja na ugawaji wa ardhi kwa maeneo yaliyofutwa hati na na muheshimiwa Raisi. Uzalishaji na udhibiti wa mifumo ya kilimo, kwani kilimo cha kisasa kinahitaji sana pembejeo, ambapo alisema inabidi kuwa makini ili kujua ni aina gani ya kilimo tunakitaka ili kufanya uzalishaji kuwa endelevu. Suala la fedha kwaajili ya uendeshaji ni tatizo. Masoko kwa wakulima imekuwa ni shida na tatizo hasa lipo kwenye usambazaji na sio uhitaji. Mipango inayofanyika inazingatia ASDP 2 na utekelezaji wake unaendana na kile kinachofanywa na serikali.

“Taasisi ina mapango wa kufungua redio yake ili kufanya sauti ya mkulima isikike. Pia tuna mpango wa kufungua kiwanda cha uchakataji mazao, tunaamini kuwa siku kutakuwa na kiwanda hicho na kitafanya kazi. Kama ilivyokuwa mwanzo wakati tuanza shirika hili.Tulianza kidogo na kulikuwa na changamoto nyingi lakini sasa tumefika hapa ni kwasababu ya kuishi katika ndoto zetu”Stephen Ruvuga

Aidha alihitimisha kwa kusema kuwa” Changamoto zipo, katibu mkuu ni mtafiti wa ardhi na unaelewa changamoto na sheria za ardhi. Tunaamini kuwa utafiti wako utatusaidia. Tunashukuru kwa kututembelea MVIWATA licha ya majukumu uliyonayo”

Baada ya utangulizi wa Mwenyekiti na Mkurugenzi ukafika wasaa wa mgeni rasmi kutoa yake machache kwa hadhara iliyokuwepo.

“Ninashukuru nipo nyumbani. Mwenyekiti na Mkurugenzi mmesema mazuri kunihusu na ninashukuru. Sifa ziwaendee watanzania kwa kunisomesha kwa kodi zao hatimaye nikaweza kupata shahada zote tatu na siwezi kuwasahau watanzania. Nina deni kubwa la kulipa utumishi uliotukuka. Kazi niliyopewa kuwa mtendaji wa chama kinachoongoza serikali ni jukumu kubwa mno”

Katika maelezo yake katibu mkuu alisema inabidi kufanya tafiti zitakazotatua changamoto za wafanyakazi na wavuja jasho na kutafuta majawabu katika eneo la uzalishaji mali. Kwani katika maeneo hayo kuna mambo ambayo bado hayajafanyiwa kazi ya kutosha. Lazima kuwe na misingi ya kutetea  haki za wanyonge na kusimamia utu.

Katibu mkuu aliongeza kuwa kama taifa bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kulinda wafanyakazi, kwasababu kumekuwa na dhuluma na unyonyaji. Sera ni miongoni mwa vitu vinavyokwaza juhudi za kujiendeleza hasa kwa watu wa kipato cha chini ambao ni wazalishaji wadogo. Ili kuweza kuwa na maendeleo amewataka wakulima kuunda chombo cha kujitetea ili kukata minyororo na mirija ya unyonyaji. Kwani serikali haiwezi kusikiliza mahitaji ya mtu mmoja mmoja hivyo ni lazima wawe na chombo cha kuwapazia sauti.

Nidhamu na uwajibikaji ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya taasisi yoyote “Miaka ishirini na tano imewasaidia sana kupunguza madhila yenu. Vyombo hivi vinapaswa viwe na nidhamu na wa watumishi ni lazima wawajibike ipasavyo. Sio hivyo tu bali viongozi wawe madhubuti katika usimamizi mzuri wa vyombo vyao na wasijiingize katika siasa. Nimedhamiria kupambana na ufisadi na unyonyaji dhidi ya wazalishaji wadogo. Msione haya kupaza sauti kwa kiongozi anayewatetea” Dokta Bashiru.

Ametahadharisha kuwa Afrika inanyemelewa na ukoloni mpya ili kudhibiti rasilimali zake. Hasa ardhi na vilivyomo. Watu wanaoweza kutulinda dhidi ya ukoloni huu ni wakulima wadogo wadogo,ambao ndio watumiaji wakuu wa ardhi. Bado azimio la Arusha lina mashiko mpaka sasa.

Ameiasa taasisi ya MVIWATA kuzingatia mambo mbalimbali katika utendaji wake ikiwemo kuwa chombo kinachowajibika, mtazamo wa kujitegemea, kuwekeza katika rasimali watu, watumishi kujitoa zaidi kwa kufanya kazi zaidi, kuacha uroho na ubinafsi, kuchagua aina ya misaada kutoka kwa wahisani, lazima kujua lengo la muhisani katika msaada anaoutoa na pia kuwalinda wafanyakazi kwa kuwapa maisha ya staha.

Ameeleza kuwa uwepo utaratibu mzuri wa mawasiliano kupitia ofisi ili MVIWATA iwe kama daraja la serikali na wavuja jasho. Mtandao huu upanuke usiwe wa wakulima pekee bali kuwe na mtandao wa wavuvi na wafanyabiashara pia. Amependekeza kuwa katika mkutano mkuu kuwe na mijadala zaidi na sio hotuba ili watu waweze kutoa hoja na mitazamo yao. kama ikiwezekana na wao kama serikali wapate mualiko ili washiriki katika majadiliano hayo.

MVIWATA ni taasisi ya wakulima hivyo wakulima nao walipewa kipaumbele katika kuwasilisha kero zao kwa mgeni rasmi ambapo waliuliza maswali tofauti mengi yakilenga changamoto za ardhi na masoko.

Bi.Arafa Simba kutoka Kilosa aliwasilisha kero kati ya Halmashauri ya Wilaya na wananchi ambao bado hawajakabidhiwa hati za shamba lililogawiwa kutoka kwa mwekezaji na hivyo wao kukosa ardhi ya kufanya shughuli za kilimo. Hivyo kumuomba Katibu Mkuu awasaidie katika suala hili waweze kupata ardhi na kuendelea na shughuli zao.

Richard Hanga kutoka Kilombero alieleza kuwa kumekuwa na mgogoro wa ardhi kati ya kijiji na kampuni ya uzalishaji sukari ya Kilombero Plantation Limited (KPL). Ambapo kampuni hiyo ilifanya utanuzi wa mipaka na kuchukua sehemu ya ardhi ya wanakijiji. Huku wananchi wakibaki bila ardhi, amemuomba katibu mkuu kusaidia kutatua mgogoro huo.

Iddy Ally kutoka wilaya ya Kilosa alitoa changamoto yake kuwa wamezuiliwa kufanya kazi katika eneo ambalo liligawiwa kwa wananchi na kisha likarudishwa kwa mwekezaji. Mpaka sasa hawana ardhi ya kulima na kumekuwa na vitendo vya kinyanyasaji kwa wananchi vinavyofanywa na walinzi wa mwekezaji huyo.

Frolence Haule kutoka Ruvuma alitoa kero yake ya kuwepo kwa wawekezaji wanaohodhi maeneo makubwa. Wamepeleka matatizo yao kwa viongozi wa serikali lakini kumekuwa na mwitikio hasi katika suala lao. Hivyo ameomba serikali itafute mwarobaini wa kero hii kwani wananchi hawana ardhi ya kulima.

Zainabu Kisegere kutoka wilaya ya Kilosa kata ya Msowelo amesema serikali ilirudisha ardhi kwa wananchi lakini wilaya imechukua hiyo ardhi tena na kuigawa kwa wageni. Hivyo anashindwa kuilewa wilaya kwa kushindwa kusimamia ardhi hiyo na kutaka maelezo kutoka kwa katibu.

Bi. Otensia Thomas kutoka Morogoro alitoa kero yake ya baadhi ya watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Morogoro vijijini kuchukua vyanzo vya mapato ya masoko yaliyojengwa na MVIWATA pamoja na unyanyasaji kwa wananchi. Hivyo anaomba serikali iwasaidie kuondokana na kero hii.

Jeremia Maina kutoka Dodoma amemuomba Katibu Mkuu kuwashughulikia watumishi wa serikali wanaosema kuwa wakulima hawana weledi na viongozi ambao ni kero kwa wananchi hali ambayo imesambaratisha na kuvunja umoja wa wakulima wadogo katika kijiji cha Kibaigwa.

Katibu Mkuu alijibu kero hizo kwa kutoa maelezo ya jumla. Alieza kuwa “nawashukuru kwa kuwa wa wazi. Dhana ya uwekezaji wa maana wenye manufaa na unaojenga uchumi wa kitaifa ni ule wenye uhusiano na uzalishaji. Uwekezaji katika Afrika umekuwa wakiporaji. Katika mazingira ya kiafrika mwekezaji ni mkulima. Mwekezaji anayezalisha kwaajIli yake na kutoa ziada katika uchumi ni mkulima. Kama unatafuta sekta halisi katika uchumi wetu ni sekta ya kilimo. Sahau amani kama hutadhibiti rasilimali ya ardhi. Mchakato wa ardhi popote ulipo usimame tujiridhishe kama ushirikishwaji ulitosha. Amekiri kuwa ardhi zilizotwaliwa na Raisi bado zina utata. Ninaomba myaandike haya mliyoyasema kwa vielelezo na ushahidi wenye viambatanisho tutatoa majawabu”

“Kuhusu suala la masoko andikeni barua ipelekwe kwa Waziri wa TAMISEMI. Serikali chini ya Mheshimiwa Raisi haitabadilisha msimamo wa kuwatetea wafanyakazi na wakulima. Niwatie moyo kuwa siku zote tabia ya mtu mnyonyaji ni maneno ya kebehi hivyo msikatishwe tamaa na maneno hayo. Tukigundua unadhalilisha wakulima tutakuchukualia hatua”.

Amehitimisha kwa kuwashukuru wananchi kwa niaba ya Raisi na kusema kuwa pongezi zinazotolewa zinawajenga na kuwafanya waone kuwa wana deni kubwa la kuwalipa watanzania. Na pia amepokea taarifa na mapendekezo yaliyotolewa na kuahidi kuwa serikali itayafanyia kazi ili kutetea maslahi ya wavuja jasho.

Mviwata on Facebook

Subscribe to our monthly newsletter