ZAIDI YA WANANCHI 200 WAPATIWA HUDUMA ZA KISHERIA JUU YA ARDHI WILAYANI KILOSA MKOANI MOROGORO.

Zaidi ya wananchi 200 kutoka vijiji vya Msowero na Mambegwa wilayani Kilosa mkoani Morogoro wamepatiwa huduma ya msaada wa kisheria juu ya masuala mbalimbali yanahusu ardhi kutoka kwa wanasheria wa mtandao wa vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) kwa lengo la kupunguza migogoro ya mara kwa mara ardhi ambayo imekuwa sugu wilayani humo hatua inayopelekea vifo pamoja na ulemavu wa kudumu miongoni mwa wananchi.

Kayunga Yango ni mwanasheria wa Mtandao wa Vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) amesema wameandaa mpango huo kwa lengo la kuwajengea uelewa wananchi kuhusu masuala ya ardhi kutokana na idadi kubwa wa wakazi hao kushindwa kufahamu wajibu wao kisheria hatua inayopelekea wengi wao kupoteza haki zao za msingi kutokana na kutojua sheria hatua inayopelekea kuingia kwenye migogoro isiyo kuwa na tija kwa taifa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa MVIWATA Stepehen Ruvuga amesema wanaishukuru serikali ya awamu ya tano chini ya Raisi Magufuli kusikiliza kilio cha wakulima na kuamua kufuta mashamba pori ambayo yalikuwa hayaendelezwi kwa muda mrefu huku pia akibainishwa kuwa kwa sasa ni utekelezaji tu ugawaji wa mashamba hayo kuzingatiwa ili kuwawezesha wananchi wote kunufaika na mashamba hayo.

Ruvuga amesema MVIWATA wataendelela kutoa huduma hiyo ya kisheria na  sehemu nyingine nchini kwa lengo la kuwawezesha wakulima walio wengi kujua na kutambua haki zao kisheria kuhusu masuala ya ardhi ikiwa ni sehemu moja wapo ya kuunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano juu ya kutokomeza migogoro ya ardhi inayotokea mara kwa mara katika wilaya za Kilosa na Mvomero.

Katika utoaji huo wa msaada wa kisheria jumla ya wanasheria watano kutoka MVIWATA  waliweza kufika maeneo hayo ya Mambegwa na Msowero  na kutoa huduma hiyo  ya msaada wa kisheria juu ya ardhi na mirathi kwa mtu mmoja mmoja pamoja na kusikiliza shida ya pamoja huku idadi kubwa ya watu wakijitokeza kupata huduma.

MWISHO

Mviwata on Facebook

Subscribe to our monthly newsletter