Tarehe 17 April 1996 wakulima 19 waliuawa na dola katika nchi ya Brazil wakiwa katika harakati za kutetea ardhi yao. Tunaungana na wakulima wadogo duniani kote katika kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Mapambano ya Wazalisahji Wadogo Duniani.
Watu hao 19 waliopoteza maisha yao ni mashahidi wa mapambano ya kupigania haki za wanyonge na mauaji yao ni ushuhuda wa madhila, mateso na hatari tanazokumbana nazo wakulima katika kudai haki yetu.
Hivi karibuni tumeshuhudia ongezeko la harakati za uporaji wa ardhi kwa kisingizio cha uwekezaji. Katika nchi yetu harakati hizo zimepelekea msukumo wa kutaka kubadili sera na sheria ili kurahisisha uporaji wa ardhi kinyume na maslahi ya wakulima wadogo na kwa ujumla kinyume na maslahi ya taifa letu. Mabadiliko yoyote ya sera na sheria yenye lengo la kuiondoa ardhi kutoka katika umiliki wa jamii pana wakiwemo wakulima wadogo na kuikabidhi ardhi hiyo kwa wachache hususani makampuni au matajiri wachache ni hatari kwa mmomonyoko wa amani yetu na taratibu yanaturejesha katika mifumo ya kinyonyaji na kitabaka ambayo taifa letu lilipambana kwa nguvu zote kuondokana nayo.
Leo hii katika sehemu mbali mbali za nchi yetu kuna shuhuda za wakulima wadogo kunyanyaswa, kutishwa, kubambikiziwa kesi ili mradi tu tukate tamaa ili kuruhusu uporaji wa ardhi kwa maslahi ya wachache.
Tunawapongeza wakulima wote waliosimama kwa mshikamano kupinga uporaji wowote wa ardhi.
Rai yetu kwa wazalishaji wadogo kote nchini ni kuendelea kusimama na kutetea haki na usawa, kupambana na kutokomeza maovu na madhila yoyote yenye nia na malengo ya kutunyonya ili tuweze kuwa na mazingira bora ya kuzalisha chakula kinacholisha Taifa na kujenga jamii yenye haki na usawa.
Mfumo wa uzalishaji ni lazima ujengwe juu ya misingi ya haki, usawa, heshima na kutoa ulinzi kwa wazalishaji wadogo ambao siku zote tumekuwa nguzo ya uzalishaji chakula na mazao mengine katika taifa letu na huu ndiyo mfumo sahihi kwa taifa letu.
Tunatumia fursa hii kuishurukuri Serikali yetu kwa kupigia Kura Azimio la Umoja wa Mataifa la Wakulima Wadogo katika mkutano wa Baraza la Umoja wa Mataifa. Tunatumaini kwamba Serikali yetu italisimamia na kuliheshimu Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Wakulima Wadogo ili kuhakikisha wazalishaji wadogo nchini wanapata haki na usawa kama ilivyoainishwa kwenye azimio hilo.
“Mtetezi wa Mkulima ni Mkulima Mwenyewe”





