Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) iliandaa kongamano la kumbukumbu ya aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani Edward Moringe Sokoine. Kongamano lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Jordan mjini Morogoro. Lengo la kutaniko ni kuchambua fikra, maisha na mtazamo wa Sokoine katika ujenzi wa Uchumi wa kitaifa na hasa maendeleo vijijini.
Watoa mada walikuwa ni Dr. Bashiru Ally, Prof. Issa Shivji mada ambazo zilijadiliwa na wanachama wa MVIWATA. Wageni wengine waalikwa walikuwa ni mashirika rafiki na waandishi wa habari. Mada zilizojadiliwa ni Ni nani hasa Sokoine iliyowasilishwa na Dk. Ng’wanza Kamata mhadhiri kutoka chuo kikuu cha Dar es Salaam, mada ya pili ni Fikra, Mtazamo na Maisha ya Sokoine katika Muktadha wa sasa wa Taifa iliyowasilishwa na Dk. Bashiru Ally, vile vile mada ya Ushirika na Maendeleo iliwasilishwa na Pro. Issa Shivji Mkurugenzi Mtendaji wa KAVAZI la Mwalimu.
Dk. Kamata alimuelezea Sokoine kama kiongozi makini, aliyeishi maisha ya kawaida kupita kawaida. Aliendelea kwa kusema kuwa Sokoine hakuwa muoga wa kuamua jambo wakati hata kama lina kinzana na sheria. “Ni mtu ambaye alipenda kujadiliana zaidi na sio kuamrisha. Alimuheshimu mkubwa kwa mdogo na hakupenda kujilimbikizia mali”.
Katika kujadili fikra, maisha na mtazamo wa Sokoine katika muktadha wa sasa Dr. Bashiru Ally anasema “Adui wa haki na usawa ni wizi na unyonyaji, havikai pamoja hivi na fikra za Sokoine ni dhidi ya watu wenye nguvu kisiasa lakini wanaodokoa na kuiba mali za umma. Jamii ya kinyonyaji haiwezi kusimamia mali za umma. Rushwa, Ufisadi na Unyonyaji ni mapacha. Ubaguzi unatokana na jamii ambayo haina usawa. Sokoine hakuwa muoga alipambana na wanyonyaji. Wakati wa Sokoine ilikuwa unachagua kama unataka kufanya biashara au unataka kufanya siasa”. Dr Bashiru alisisitiza kuwa Sokoine alikuwa na bahati ya kufanya kazi na Mwalimu Nyerere ambapo wote waliamini kwa dhati katika Azimio la Arusha.
Washiriki walipata fursa ya kujadili fikra za Sokoine na mchango wake katika ujenzi wa maendeleo vijijini ambapo walitoa changamoto zinazowakabili ikiwemo migogoro ya ardhi, masoko, vipimo vya mazao, unyonyaji pamoja na ubadhirifu kwa viongozi wa umma katika maeneo yao. Vile vile washiriki walisisitiza juu ya umuhimu wa kuwa makini katika kuchagua viongozi wanoguswa na changamoto za wananchi na sio wale wanaotaka kujinufaisha kibinafsi.
Prof Shivji katika kuchangia mjadala alisema hatuwezi kujikomboa bila mapambano. “Tuhakikishe tunatumia mkutano mkuu wa kijiji na halmashauri ya kijiji. Tukiona viongozi wakijiji hawatekelezi tunayowaambia tunawafukuza. Pili tunahitaji chombo cha ushirika, ushirika ambao utakuwa na sura tofauti, ushirika utakaokuwa wakidemokrasia. Ushirika ambao utatafuta masoko na kuendeleza viwanda vidogodogo. Ushirika ambao mfumo wake utatoka chini kwenda juu” alisema Prof Shivji.
Katika kuhitimisha majadiliano Dr Bashiru aliisihi MVIWATA kuendelea na utaratibu wa kukutana na kujadiliana, pili kuendeleza mapambano kwa kutambuana kitabaka na sio kinasaba na tatu kuendelea kuelimishana kwa kupitia njia za kisasa zinazoendana na teknolojia ya sasa na vile vile kuelimishana juu athari za unyonyaji na mbinu mbalimbali za kinyonyaji zinazotumika.
Edward Moringe Sokoine alifariki kwa ajali ya gari tarehe 12/4/1984 akitokea Dodoma kwenda Dar es salaam. Sokoine atakumbukwa daima kwa uchapakazi wake na mchango wake katika Ujenzi wa Uchumi wa Kitaifa na hasa maendeleo vijijini.





