MVIWATA kwa kushirikiana na taasisi ya HAKIARDHI na TAGRODE chini ya AllianceTALA wamefanya Mdahalo na wananchi wa Kijiji cha Kichangani, Wilaya ya Ulanga, Morogoro uliohusu Sera na Sheria za Ardhi kupitia Programu ya LTSP (Land Tenure Support Program). Mgeni Rasmi wa mdahalo alikuwa ni Mkuu wa Wilaya ya Ulanga aliyewakilishwa na Afisa Tawala wa Wilaya.
Kupitia mdahalo sera ya ardhi iliwasilishwa na wanasheria kwa wananchi ambapo nao pia walitoa maoni yao zikiwemo kero mbalimbali za migogoro ya ardhi katika maeneo yao. Baadhi ya kero hizo ni pamoja na mabadiliko ya mipaka ya vijiji bila ushirikishwaji wa wananchi, viongozi wa serikali ya kijiji kutokuwa na ushirikiano na wananchi na baadhi ya wananchi kutokupimiwa mashamba yao huku wengine wakilalamikia sera za uwekezaji kupora maeneo makubwa ya ardhi na hivyo kuwaacha wananchi wenye kipato cha chini bila ardhi ya kutosha kukidhi mahitaji yao.
Akitoa majibu kwa mamia ya wananchi wa Kichangani, Katibu tawala wa wilaya ya Ulanga aliwasihi wananchi kushiriki mikutano mikuu ya vijiji pamoja na kuhakikisha wanachagua viongozi watakaowajibika kwao kikamilifu. Vilevile aiwasihi wananchi kuandika barua kwa Mkuu wa Wilaya ya Ulanga na kuorodhesha kero zao zote na kuzifikisha Ofisi za Wilaya ili Mkuu wa wilaya aone haja ya kutembelea kijiji cha Kichangani na kuongea na wananchi kwa nia ya kutatua changamoto zilizopo.
Awali kabla ya siku ya mdahalo washiriki kutoka MVIWATA, TAGRODE na HAKIARDHI kupitia AllianceTALA pamoja na wananchi wa Kata ya Kichangani walitembelea maeneo yenye migogoro ya Ardhi ikiwemo msitu wa uliohifadhiwa wa Chokoachoka uliopo kata ya Kichangani kwa ufahamu zaidi.
Mara baada ya mdahalo wanasheria kutoka MVIWATA na HAKIARDHI waliendelea na utoaji wa Huduma ya Msaada wa Kisheria kwa siku tatu zaidi kwa wananchi katika Vijiji vya Igumbiro, Kichangani, Chilombola na Mzelezi viivyopo katika Wilaya ya Ulanga.
MWISHO





