Balozi wa Ireland Nchini ndugu H:E Paul Sherlock April 17 mwaka huu 2018 ametembea ofisi za mtandao wa Vikundi vya wakulima Tanzania (MVIWATA) ngazi ya kati Shinyanga kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayoendeshwa na mtandao huo wa kulima na kufadhiliwa na ubalozi huo Ireland.
Katika Msafara huo Balozi ameambatana na maafisa wengine wawili kutoka ubalozi wa Ireland pamoja na viongozi wa mkoa wa Shinyanga akiwemo Katibu tawala ambaye amemuwakilisha mkuu wa mkoa, afisa kilimo wilaya, afisa kilimo Manispaa, afisa elimu mkoa na viongozi wengine, huku kwa upande wa MVIWATA mkurugenzi ndugu Steven Ruvuga pamoja na mjumbe wa bodi ndugu Charles Ndugulile wakiambatana na viongozi wa ngazi ya kati Shinyanga pamoja na baadhi ya wanachama kutoka kata ya LUBAGA walishiriki katika tukio hilo la kuwapokea wageni huo kutoka ubalozi wa Ireland.
Katika hotuba yake balozi Paul ameupongeza uongozi wa MVIWATA kwa kufanya kazi kwa ukaribu zaidi serikali pamoja na vikundi vingine hatua ambayo inasaidia kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima kwa urahisi zaidi kutokana na kuwa wa moja licha ya ugumu uliopo katika sekta hiyo huku ukisema kazi inayofanya na MVIWATA ni muhimu sana katika jamii pamoja na taifa kwa ujumla.
Balozi Paul amesema sekta ya kilimo ni sekta ngumu inayohitaji kujizatiti hasa kukabiliana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya ukosefu wa masoko kwa mazao mbalimbali ya wakulima, ukosefu wa mbegu bora pamoja na changamoto mbalimbali za ulizashaji ambazo wakulima wamekuwa wakikumbana nazo kila kukicha huku akisema kuwa kilimo ni uti wa mgongo kwa taifa hivyo wakulima hawana budi kufundishwa zaidi juu ya kilimo cha kisasa chenye tija kwa taifa.
Balozi hakuishia hapo bali pia amewataka wanachama na viongozi wa MVIWATA kuendelea kufanya kazi ya kwa kujituma zaidi na kuendelea kutoa misaada mbalimbali kwa wakulima licha ya uwepo wa baadhi ya changamoto ambazo zimekuwa zikirudisha nyuma juhudi za mtandao huo lakini amewataka kuacha kukata tamaa kutokana na kazi wanaoifanya kuwa ya muhimu sana katika jamii inayowazunguuka huku pia akisema ubalozi huo utaendelea kufanya kazi na MVIWATA kwa pamoja kwa lengo la kuangalia namna gani ya kuweza kuboresha sekta hiyo ya kilimo kutokana na kuwa na umuhimu mkubwa katika jamii na taifa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mviwata ndugu Stephen Ruvuga umeushukuru ubalozi huo wa Ireland kwa kuendelea kushirikiana MVIWATA katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo yenye lengo la kumkomboa mkulima ili naye kunufaika na matunda ya kilimo chake, huku akisema Mviwata itaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa jamii katika nyanja tofauti kwa lengo la kuhakikisha mkulima anapiga hatua kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine kimaendeleo.
Wageni hao Kutoka nchini Ireland wametembelea ofisi ya Mviwata kanda ya kati Shinyanga ambayo ipo jengo la Pamba mkoani Shinyanga pamoja na kusikiliza baadhi ya changamoto zinazowakabili wanachama ngazi ya chini yaani kata ya Lubaga pamoja na ngazi ya mkoa wa Shinyanga.
MWISHO





