MVIWATA YAFANYA UFUATILIAJI WA UTEKELEZAJI WA KAMATI ZA UMAPESA, KATA YA KISAKI, MOROGORO VIJIJINI.

Mtandao Wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) umefanya zoezi la ufuatiliaji wa utekelezaji wa kamati za UMMAPESA (PETS) yaliyotolewa kwa wakulima 124 katika Kata ya Kisaki, Wilaya ya Morogoro Vijijini.

Ufuatiliaji huo umefanyika katika vijiji vinne vya Kisaki station, Nyarutanga, Gomero na Kichangani. Ufuatiliaji ulilenga kubaini changamoto za utekelezaji wa UMMAPESA na kutafuta suluhisho za changamoto zilizojitokeza kwa ustawi endelevu wa wananchi.

Katika ufuatiliaji wakulima wameeleza hatua walizofikia na changamoto walizokumbana nazo katika ufuatiliaji wa miradi mbali mbali inayoendelea katika vijiji vyao

Awali kabla ya kuelezea changamoto za ufuatiliaji huo, wakulima walibainisha miradi mbali mbali waliyokuwa wakiifuatilia kama ifuatavyo; miradi ya maji, uvunaji wa mbao, ujenzi wa nyumba za waalimu, ujenzi wa nyumba za madaktari, ujenzi wa nyumba za madaktari, ujenzi wa ofisi za vijiji na ujenzi wa vyoo katika shule za msingi.

Katika kuelezea changamoto hizo, ushirikiano hafifu baina ya viongozi wa serikali za vijiji na uelewa mdogo wa wanakijiji katika kutambua umuhimu wa mkutano mkuu wa kijiji kama msingi mkuu wa maamuzi ya maendeleo ya kijiji kumechangia kwa kiasi kikubwa katika ubadhirifu wa mali za umma.

Ushirikiano mbaya kati ya viongozi wa serikali ya mkoa, wilaya na vijiji katika kubuni na kutekeleza miradi ilikuwa ni changamoto nyingine iliyoibuka katika ufuatiliaji huo. Hatua hiyo imepelekea viongozi wa vijiji pamoja na wanakijiji kutokuwa na taarifa sahihi za miradi mbali mbali inayoendelea katika vijiji vyao hivyo kukosa taarifa za miradi ambayo imesimama kwa mda mrefu katika vijiji vyao na kutokujua ni lini miradi hiyo itakamilika.

Licha ya changamoto zote hizo walizokumbana nazo, wakulima hao wameishukuru taasisi ya MVIWATA katika kutoa elimu ambayo imewafungua macho ya kuhoji, kupata taarifa na kuona jinsi wanavyoweza kunufaika na miardi mbali mbali inayoendelea katika vijiji vyao. Pia wamesisitiza kuendelea kufuatilia taarifa zaidi kuhusu miradi hiyo pamoja na kuendelea kusambaza elimu ya uraia kwa wananchi wengine ili kujua haki na wajibu wao kama raia.

Wakihitimisha mawasilisho yao, wakulima hao wameazimia kuendelea kuwaelimisha wananchi wengine katika maeneo yao ili kutambua umuhumu wa kuhudhuria mikutano mikuu ya kijiji kwa sababu nidpo mipango ya maendeleo na taarifa mbali mbali za kimaamuzi zinapopatikana, hivyo ushiriki wao utawapa nafasi ya kuhoji mambo mbali mbali yanayoendelea katika vijiji vyao.

Mwisho wameiomba MVIWATA kuendelea kuwapa elimu ya uraia ambayo imewasaidia kupata njia bora za ufuatiliaji wa mali za umma pamoja na ushiriki wao katika maendeleo.

 

Mviwata on Facebook

Subscribe to our monthly newsletter