MKUTANO MKUU WA DHARURA MVIWATA NGAZI YA KATI KAGERA WAFANYIKA

Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) ngazi ya kati Mkoa wa Kagera wafanya mkutano mkuu wa dharura. Mkutano huu umefanyika tarehe 5 Julai 2018 katika ukumbi wa ELCT Hotel Bukoba na ulihudhuriwa na wajumbe 92 (wanawake 37 na wanaume 55) kutoka wilaya za Muleba, Ngara, Kyerwa, Misenyi na Bukoba Vijijini. Mkutano huu umefanyika kwa mujibu wa katiba ya MVIWATA ikiwa na ajenda za Kufungua Mkutano Mkuu wa Dharura, Salamu za Serikali, Kujadili Maendeleo ya MVIWATA Kagera, Kupokea na kujadili taarifa ya ukaguzi wa ndani wa MVIWATA Kagera, Uchaguzi wa kamati ya uongozi na Kufunga Mkutano.

Katika uwakilishi wa serikari Katibu Tawala wa Wilaya ya Kyerwa Ndugu Greyson Mwengu alitoa nasaha zake kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa ambaye ndiye aliyekuwa mgeni mwalikwa wa mkutano huo lakini hakuweza kufika kutokana na kubanwa na shughuli mbalimbali za serikali.

Ndugu Mwengu kwanza alitoa shukrani kwa kuialika serikali katika mkutano huo. Akitumia kaulimbiu ya mkoa ya “Kazi, Amani na Maendeleo” Ndugu Mwengu alibainisha kwamba kwa kupitia kwa haraka haraka ameona kwamba malengo ya taasisi ya MVIWATA ni mazuri kwani ni ya kuunganisha wakulima kama lilivyo lengo la serikali.  Alieleza kwamba katika mkoa wa Kagera kilimo ni shughuli muhimu sana hasa la zao la kahawa. Aliitaka MVIWATA kujielekeza katika zao la kahawa katika shughuli zake katika mkoa wa Kagera. Amesisitiza ushirikiano katika shughuli za kiuchumi kwa wakulima kwa maslahi ya wakulima na kwa maslahi ya nchi.

Pia ameipongeza MVIWATA kwa kutekeleza kwa vitendo sera za Serikali kwa kuwaunganisha wakulima wadogo katika vikundi na mitandao ili kujipatia maarifa, kubadilishana mawazo na kuwa na sauti ya pamoja katika kutetea maslahi yao kiuchumi na kijamii. Alibainisha azma ya Serikali katika wilaya ya Kyerwa kuiunga mkono MVIWATA katika jitihada za kuwaendeleza wakulima.

Katika mkutano huo kulikua na majadiliano kuhusu maendeleo ya  MVIWATA katika Mkoa wa Kagera ambao ulianza kwa maelezo mafupi ya historia ya MVIWATA –Kagera tangu kuanzishwa kwake mwaka 2004 mpaka sasa, mafanikio, changamoto na jitihada ambazo MVIWATA Taifa ilifanya ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizojitokeza ndani ya MVIWATA ngazi ya kati Kagera. Maelezo hayo yalitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA, Ndugu Stephen Ruvuga.

Baada ya majadaliano, wajumbe walieleza kusikitishwa na mwenendo wa viongozi wa tawi la MVIWATA-Kagera kwa kuchochea migogoro na migawanyiko katika taasisi na kutowaheshimu wanachama.  Wajumbe pia walijadili kukiukwa wazi misingi na maadili ya MVIWATA hivyo kuazimiwa kuvuliwa uanachama kwa baadhi ya viongozi.

Vilevile Wajumbe wa mkutano huo waliazimia Ofisi za MVIWATA ngazi ya kati Kagera zihamishiwe katika Mji wa Bukoka kutoka Muleba ili ziweze kuwa karibu zaidi na wanachama walio katika wilaya mbalimbali za Mkoa wa Kagera kutokana na mazingira ya Kijiographia ya Mkoa huo. Azimio hilo lilikuja baada ya wajumbe kupiga kura ya kukubali kuhamisha ofisi hizo.

Vile vile Mkutano huo wa dharura ulifanya Uchaguzi wa viongozi wapya wa MVIWATA ngazi ya kati Kagera ambapo wajumbe tisa wa kamati ya uongozi walichaguliwa kutoka wilaya nne za Mkoa huo, Wilaya hizo ni Muleba, Ngara, Bukoba Vijijini na Kyerwa. Baada ya safu kukamilika wajumbe wa kamati mpya ya uongozi walikaa ili kuchagua viongozi wa Kamati ya Uongozi  ambao ni  Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti, Katibu na Mtunza Hazina. Hatimaye, uchaguzi ulikamilika ambapo safu kamili ya uongozi wa MVIWATA Kagera ilipatikana kama ifuatavyo;

  1. Josias Kagoma                                   Mwenyekiti
  2. Selemani Sadiki                                 Makamu Mwenyekiti
  3. Abadini Rwakibanda                       Katibu
  4. Jirian Rajabu                                       Mweka Hazina
  5. Adelina Meshack                             Mjumbe
  6. Grace Bitegeko                                 Mjumbe
  7. Prosper Mukiza                                Mjumbe
  8. Mariagorethi Gabriel                      Mjumbe
  9. Teddy Innocent                                Mjumbe

MWISHO.

 

Mviwata on Facebook

Subscribe to our monthly newsletter