Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA) umeendesha semina iliyokua na lengo la kutoa elimu juu ya mimea iliyobadilishwa vinasaba (GMO’s) kwa wabunge wa kamati ya kilimo, mifugo na maji pamoja wenyeviti wa kamati za kudumu za bunge za bajeti, biashara na miundominu. Pia kulikuwa na wadau kutoka taasisi za kilimo za serikali na zisizo za serikali pamoja na wakulima katika semina hiyo iliyofanyika mjini, Morogoro.
Akiwakaribisha katika semina hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA Ndg, Stephen Ruvuga alimshukuru Mhe. Spika Ndg, Job Ndugai kwa kuwapa fursa wabunge kuhudhuria katika semina hiyo na kuwataka washiriki kutoa michango yao na uzoefu wao juu ya mimea iliyobadilishwa vinasaba ili kujenga uelewa mpana hivyo kuwasaidia wabunge kutoa maamuzi yatakayoleta tija kwa wakulima nchini.
Semina hiyo ilihusisha watoa mada mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi. Kutoka ndani ya nchi kulikuwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) iliyowakilishwa na Dr. Nyange, Taasisi ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) iliwakilishwa na Dr, Patrick Ngwediagi, Kituo cha Utafiti wa Mazao ya Kilimo cha Mikocheni (MARI) iliyowakilishwa na Ndg, Joseph Ndunguru, Dr. Richard Mbunda kutoka Chuo Kikuu cha Dar-es-salaam na kutoka nje ya nchi alikuwepo Dr. Angelica Hilberck kutoka Kituo cha Tafiti za Kibaiolojia, Zurich Switzerland.
Wataalamu hao walielezea mitazamo yao mbalimbali juu ya mimea iliyobadilishwa vinasaba ambapo wawakilishi kutoka COSTECH, TOSCI na MARI walieleza kuwa mimea hiyo ni njia muafaka ya kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na yenye tija kwa mkulima mdogo katika uzalishaji wake kutokana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa nchini.
Dr. Mbunda alieleza kuwa mimea iliyobadilishwa vinasaba sio chaguo sahihi kwa uhuru na usalama wa chakula. Vilevile tafiti zinaonesha kuwa vyakula vya mimea hiyo havina ladha nzuri kulinganisha na vyakula vinavyotokana na mbegu za asili. Mtaalamu huyo alisisitiza kuwa mimea hiyo itajenga utegemezi wa pembejeo za kilimo (mbolea, mbegu na madawa) kutoka kwa makampuni makubwa ya kibepari.
Dr. Angelica alielezea dhana na chimbuko la GMO na kusisitiza kuwa tafiti zinaonesha kuwa hakuna uhusiano kati ya matumizi ya GMO na ongezeko la uzalishaji wa mazao ukilinganisha na mbegu za asili. Pia alieleza kuwa nchi nyingi za bara la Ulaya zimepiga marufuku matumizi ya GMO na kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya kemikali katika kilimo.
Katika kuhitimisha Ndg. Ruvuga alitoa shukrani kwa wabunge na wadau waliojitokeza katika semina hiyo wakiwemo wakulima na taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali zilizohusika katika kutoa elimu na kujenga uelewa zaidi juu ya mimea iliyobadilishwa vinasaba ambayo imekua ikipokelewa kwa hisia tofauti tofauti na wadau wa kilimo nchini.
Akifunga semina hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Mgimwa alliyekuwa mwenyekiti wa semina hiyo kwa niaba ya wabunge alitoa shukrani kwa MVIWATA kwa kuwezesha semina hiyo kwa sababu imewaongezea uelewa mkubwa juu ya mimea iliyobadilishwa vinasaba. Pia aliomba semina hizo ziwe endelevu ili kundelea kuwajengea uelewa zaidi na hivyo kutoa maamuzi yatakayo leta tija kwa wakulima wadogo nchini.
MWISHO.





