Kamati ya Kudumu ya Bunge, Tawala na Serikali za Mitaa pamoja na naibu Waziri Ofisi ya Raisi TAMISEMI Mh. Josephat Sinkamba Kandege, wametembelea soko la kimataifa la Kibaigwa kwa lengo la kujionea changamoto mbalimbali za uendeshaji wa soko hilo ambalo limejengwa na MVIWATA mwaka 2004 kwa kushirikiana na serikali ya Ufaransa na kugharimu zaidi ya bilioni 1.5.
Ziara hiyo inakuja baada ya kamati hiyo ya Bunge kukutana na baadhi ya viongozi wa MVIWATA Novemba mwaka 2017 katika ukumbi wa Dodoma Hoteli akiwemo Mkurugenzi Mtendaji Stepheni Ruvuga pamoja na Mwenyekiti Mstaafu Ndugu Veronica Sophu wakiambatana na viongozi wote wa masoko yaliyojengwa chini ya MVIWATA na kubainisha changamoto wanazokutana nazo katika uendashaji wa masoko hayo ikiwemo baadhi ya halmashauri kuchukua mapato yote ya soko bila kurudisha kiasi cha fedha ambacho walikubaliana katika mkataba, hali inayopelekea bodi ya masoko kushindwa kujiendesha hatua inayopeleka masoko hayo kuchakaa ikiwemo mizani, mabati, majengo ya soko kuchakaa,na pamoja na mazingira kutokuwa rafiki kwa watumiaji kutokana na kukosa maboresho kwa muda wa mrefu ikiwemo mashine mbalimbali za kuchujia nafaka.
Akitoa taarifa fupi ya soko, Meneja wa soko la Kibaigwa Kusekwa Dalali amesema changamoto kubwa inayowakabili ni halmashauri ya wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kukusanya mapato yote ya soko na kushindwa kurudishia kiasi cha fedha walichokubaliana katika mkataba, pamoja na halmashauri hiyo kubadisha mkataba wa uendeshwaji wa soko kiholela bila kuwashirikisha upande mwingine, Kushuka mara kwa mara kwa bei za mazao ikiwemo mahindi, Mbaazi na Mpunga, kuwa na eneo dogo la soko kutokana na mahitaji ya sasa, uchakuvu wa miundo mbinu mbalimbali iliyopo sokoni ikiwemo Mizani, majengo, fensi, barabara, mashine za kusafishia mahindi, kuibuka kwa masoko holela jirani na soko, uwepo wa ukusanyaji wa ushuru kwenye njia zinazoingia sokoni hatua inayopelekea wakulima wengi kuuza mazao yao nje ya soko.
Baada ya kusikiliza taarifa hiyo fupi kamati hiyo ya bunge ukatembelea maeneno mbalimbali yaliyotajwa kwenye taarifa kwa lengo la kuhakikisha kile kilichobainishwa dodoma na taarifa iliyosomwa zina usahihi, na ndipo hapo walipogundua ukweli hatua iliyopelekea kamati hiyo kupitia kwa mwenyekiti wake msaidizi wa kamati Mh. Mwanne Nchemba ambaye pia ni Mbunge wa viti maalumu Tabora kutoa siku ishirini na moja kwa wizara ya Tamisemi kuanzia April 22 mwaka huu kuhakikisha wanatatua changamoto hiyo kwa kuwakutanisha MVIWATA na viongozi wa halmashauri ya wilaya ya Kongwa na baada ya hapo watoe taarifa kwa kamati hiyo huku pia kamati hiyo akiagiza ukarabati wa soko, mizani, eneo la maegesho ya magari pamoja mabati kufanyika haraka pamoja na kuagiza masoko holela yalipo nje ya soko la Kibaigwa kuondolewa kwa kutunga sheria ndogo ya usimamizi wa maeneo, huku pia wakiomba wizara hiyo ya Tamisemi kwa kushirikiana na MVIWATA kuipeleka kamati hiyo ya bunge katika halmashauri ya Mbalali mbeya ambayo inatekeleza mradi huo kwa ufanisi kwa lengo la kujionea na kulinganisha kwanini halmashauri ya wilaya ya Kongwa inashindwa kufanya hivyo kama halmashuri nyingine.
Kwa upande wake Naibu waziri wa TAMISEMI ndugu Josephat Kandege amesema hawezi kuliacha jambo hilo zuri kufia katika mikono yake hivyo atahakikisha atalisimamia na ndani ya siku ishirini na moja atapata jibu la uhakika kuhusu sakata hilo, huku akisema atapitia mikataba ya pande zote mbili ikiwemo MVIWATA na halmashauri ya Kongwa la kujua tatizo nini ndani ya siku hizo 21 alizopewa na kamati bunge.
Mkurugenzi Mtendaji wa MVIWATA ndugu Stephen Ruvuga amesema amepokea maagizo yote aliyopewa na kamati hiyo ya bunge kuhakikisha changamoto mbalimbali zinazojitokeza zinatatuliwa huku akisema wanajua halamashauri nyingi ziko kwenye heka heka za kukusanya mapato lakini wao kama MVIWATA wako tayari kukaa meza moja na kutoa ushauri kwa halmashauri jinsi gani ya kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Licha ya changamoto hizo lukuki uwepo wa soko la Kibaigwa umechangia kuongezeka kwa ajira Kibaigwa na katika vijiji vya jirani kupitia shughuli za sokoni, biashara mbalimbali na huduma kama za mebenki, huku pia soko hilo likiwa ni chanzo kikubwa cha mapato kwa halmashauri ya wilaya Kongwa ambapo kwa kipindi cha miaka kumi na minne (14) iliyopita yaani 2004 – 2017 halmashauri hiyo imekusanya zaidi ya shilingi 2,450,148,250/=.
MWISHO.





